Simba haikamatiki 

24Oct 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba haikamatiki 
  • ***Yapeleka tena kilio kwa Azam FC, huku Kagere akizidi kung'ara...

BAADA ya kuwafunga na kubeba Ngao ya Jamii, Simba imeendeleza ubabe kwa Azam FC kwa kupata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wachezaji wa Simba wakishangilia baada ya kupata bao katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. PICHA: JUMANNE JUMA

Mabingwa hao watetezi waliondoka na pointi tatu baada ya mshambuliaji wake Mnyarwanda Meddie Kagere kufunga bao pekee katika mchezo huo na kuifanya timu hiyo ifikishe pointi 15 na kujiimarisha katika msimamo wa ligi, baada ya kushuka dimbani mara tano.

Kagere alifunga bao hilo kwa kichwa, kufuatia krosi safi kutoka kwa pacha wake aliyekuwa naye Gor Mahia, Francis Kahata na kuujaza wavuni huku kipa, Mwadini Ally, akiruka bila mafanikio ikiwa ni dakika ya 49 na kufikisha bao la saba kwenye kibindo akikifukuzia tena kiatu cha dhahabu.

Kwa upande wa Azam yenyewe imekamilisha mechi ya nne, ikishinda tatu, na kufungwa mchezo mmoja, ikikamata nafasi ya sita.

Kipindi cha kwanza timu hizo zilionekana kucheza kwa kukamiana na ubabe, lakini hali ikabadilika kipindi cha pili, kila timu ilipoamua kutandaza kandanda safi.

Kashikashi kwenye mechi hiyo ilianza dakika ya kwanza tu wakati Msudan Sharaf Eldin Shiboub, alipoachia shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari, lakini mpira ulipaa kidogo kwenye goli la Azam.

Sekunde chache baadaye, Shiboub nusura aipatie Simba bao la mapema baada ya kuunganisha kona iliyochongwa na Gadiel Michael, lakini kabla haujavuka mstari wa goli iliokolewa kwa kichwa na mlinzi wa Azam, Bruce Kangwa na kuwa kona nyingine ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya tatu, aliikosesha Azam bao baada ya kupiga kombora kali lililotemwa na kipa Aishi Manula na baadaye kuudhibiti tena kwenye mikono yake.

Azam ilipata tena nafasi safi ya kupata bao kwenye dakika ya 37 wakati straika wake raia wa Ivory Coast, Richard Djodi alipoukuta mpira unazagaa kwenye eneo la hatari, akaachia shuti kali lililookolewa na Manula.

Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko, Simba ikiwatoa Shiboub, Kahata na Hassan Dilunga, nafasi zao kuchukuliwa na Clatous Chama, Miraji Athumani na Ibrahim Ajibu, huku Azam ikiwatoa Domayo, Joseph Mahundi, nafasi zao kuchukuliwa na Donald Ngoma na Selemani Idd "Nado", na kuufanya mpira uchangamke zaidi.

Baada ya mchezo wa jana, mabingwa hao watetezi wanatarajia kusafiri kuelekea Arusha, kuwafuata Singida United, katika mchezo mwingine wa ligi hiyo utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo.

Matokeo ya mechi nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizochezwa jana ni Alliance imefanikiwa kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza wakati Coastal Union imelazimishwa suluhu Uwanja wa Mkwakwani dhidi ya Singida United, Polisi Tanzania ikawachapa Mwadui FC bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi na Namungo ikiendelea kung'ara kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa mjini Lindi kwa kuifunga Mtibwa Sugar bao 1-0.

Tanzania Prisons yenyewe imelazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Biashara United Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, na Ndanda ikabanwa mbavu nyumbani, Uwanja wa Nangwanda Sijaona kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Lipuli FC ya Iringa.

Habari Kubwa