JKT yafanya mageuzi makubwa

24Oct 2019
Moshi Lusonzo
Nipashe
JKT yafanya mageuzi makubwa

MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Charles Mbuge, ametangaza mageuzi ndani ya jeshi hilo, na kuwaagiza makamanda wa vikosi kuwafafanulia vijana wanaojiunga kuwa hakuna ajira badala yake ni sehemu ya kupewa mafunzo ya uzalendo, ukakamavu na uzalishaji mali

Akizungumza na makamanda wa vikosi, wakuu wa vitengo na shule zinazomilikiwa na jeshi hilo,

Brigedia Jenerali Mbuge, amesema katika uongozi wake ambao una kauli mbiu “Maneno si kazi, kazi vitendo”, hautamwacha salama kiongozi atakayekwenda kinyume cha mkakati wa chombo hicho ambao ni kutoa malezi, mafunzo na uzalishaji mali kwa vijana.

Alisema katika mageuzi hayo, JKT itatekeleza kazi zake katika weledi unaokubalika, kujenga maadili kwa vijana na askari wake na uzalishaji wa chakula kwa ajili ya kuipunguzia gharama serikali.

HAKUNA AJIRA

Brigedia Jereali Mbuge alisema kuanzia mwaka huu wanafikiria kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na jeshi hilo, hata hivyo, watakaoingia katika kambi zilizochaguliwa wasiwe na fikra kwamba watapata ajira kwani hilo si jukumu lao.

“Naomba hili lieleweke na makamanda wanisaidie kutoa ufafanuzi katika jambo hili, jukumu la JKT ni sehemu ya kutoa mafunzo kwa ajili ya kuwandaa vijana kuwa wazalendo, wakakamavu, majasiri pamoja na uzalishaji mali, na si vinginevyo, sisi hatutoi ajira kama vijana wengi wanavyofikiria,” alisisitiza Brigedia Jenerali Mbuge.

Alisema katika suala hilo kuna baadhi ya vijana waliopitia jeshi hilo wamechukuliwa hatua baada ya kutumia mitandao vibaya kwa kukiuka nidhamu.

“Kuna vijana hawana nidhamu walitumia mitandao ya kijamii kwa kutoa ujumbe kwa viongozi, tumewachukulia hatua  stahiki. Pia kuna baadhi ya askari wanashindwa kutoa elimu na kuwafanya vijana kuamini JKT ni sehemu ya ajira,” aliongeza.

Alifafanua kwamba vijana hao watapata ajira endapo vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitahitaji askari kutokana na vijana hao kuwa kamili katika suala la ulinzi wa nchi. MAGEUZI UTENDAJI WA KAZI

Mkuu huyo wa JKT, alisema kuanzia mwaka huu watajikita katika kuboresha utendaji wa kazi kwa kila askari, kupanua wigo wa utoaji mafunzo kwa vijana pamoja na kuongeza uzalishaji wa chakula.

“Tunataka tufikishe malengo yetu ya kuzalisha  chakula cha kutosha kwa ajili ya vijana wetu kwa nia ya kupunguza mzigo wa gharama kwa serikali, kuongeza idadi ya vijana kujifunza uzalendo na kupanua sekta ya michezo,” alisema.

Aidha, katika kutimiza malengo ya mikakati hiyo, Brigedia Jenerali Mbuge aliwataka makamanda wa vikosi wanaoongoza idara mbalimbali kujitathmini wao wenyewe kama wanaweza kukamiliana na kasi hiyo ikiwamo kujipima kwa kazi alizofanya huko nyuma kama zimeleta tija kwa jeshi hilo.

Habari Kubwa