Waziri Mabula atuliza wananchi mgogoro na TFS

24Oct 2019
Dotto Lameck
Tanga
Nipashe
Waziri Mabula atuliza wananchi mgogoro na TFS

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angelina Mabula, amewataka wananchi wa Kijiji cha Sindeni wilayani Handeni mkoani Tanga watulie kutokana na mgogoro unaoendelea kati yao na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)kuhusu mpaka baina ya kijiji cha Sindeni na shamba la miti la Korogwe.

Mabula amewatuliza wananchi hao baada ya kufika katika shamba hilo na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi za TFS zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani Tanga.

Mabula ameiagiza idara ya ardhi katika halmashauri hiyo ikisimamiwa na Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini kuhakikisha inafanya uhakiki wa mipaka kati ya kijiji cha Sindeni na TFS na kuweka alama ili kusitisha mgogoro huo.

“Kitakachofanyika ni uhakiki ili tujue TFS wanaishia wapi na NARCO wanaishia wapi, hivyo naiagiza idara ya ardhi wilayani hapa ikisaidiwa na Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini ifanye uhakiki huo, kwa sababu tukifanya hivi tutakuwa tunaheshimu mipaka na nyaraka za vijiji vyetu’’ alisema Mabula.

Hata hivyo, wanakijiji wa Sindeni wameeleza chanzo cha mgogoro huo kuwa Wakala wa Huduma za Misiti (TFS) kuongeza eneo hadi kufika katika kijiji chao.

Mhina ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amesema “Nilimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa TFS iliacha eneo lake la asili na kuongeza eneo lingine na kuingia katika kijiji chetu akasema atalishughulikia

Naye Meneja wa Shamba la Miti la Korogwe, Pregreen Mushi, amesema, wenyeji wa Sindeni walivamia eneo la Wakala wa Huduma za Misitu huku wale wa Kwamatuko na Kwaingoma wakiuza maeneo ya hifadhi kwa jamii ya wafugaji na Mkuu wa Wilaya ya Handeni alishatoa agizo wote waliovamia kuondoka eneo la hifadhi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, amesema mgogoro huo alishaushughulikia na kuwataka ambao hawajaridhika na utatuzi huo waende mahakamani ili kufafuta suluhu ya mgogoro huo, baadhi ya wananchi walikubali kuwepo kwa msitu huo na sasa wananufaika kwa kupatiwa huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule.

Habari Kubwa