ACT-Wazalendo yakubaliwa  kesi tafsiri ukomo wa urais 

25Oct 2019
Hellen Mwango
Nipashe
ACT-Wazalendo yakubaliwa  kesi tafsiri ukomo wa urais 

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekubali ombi la Chama cha ACT-Wazalendo kujiunga kwenye kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Dezydelius Mgoya, maarufu kama Mkulima, kuhusu ukomo wa urais.

Wakili wa ACT-Wazalendo,  Jebra Kambole

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji  Dk. Benhaj Masoud baada ya kusikiliza maombi ya ACT-Wazalendo kujiunga na kesi hiyo kwa sababu wana maslahi nayo.

Wakili wa ACT-Wazalendo,  Jebra Kambole,  alidai kuwa mteja wake ameomba kujiunga kwa sababu ni chama kilichosajiliwa na kimeshiriki katika uchaguzi.

Pia alidai kuwa chama hicho kina wanachama Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar kwa mujibu wa matakwa ya kisheria na kikatiba.

Mgoya alifungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha sheria ya utekelezaji haki na wajibu, sura ya 3 ya mwaka 1994 chini ya Ibara ya 30(3) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Mgoya anahoji Ibara ya 40(20) ya Katiba ambayo imeweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano ya uongozi katika nafasi hiyo ya urais.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya Ibara ya 42(2) ya Katiba kwa kuhusianisha na masharti ya Ibara za 13, 21 na 22 za Katiba hiyo.

Kadhalika, Mgoya  anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya Ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.

Habari Kubwa