Tumeona hakuna  kama wewe UN

25Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Tumeona hakuna  kama wewe UN

UMOJA wa Mataifa (UN) sasa umetimiza miaka 74. Hongera rafiki kipenzi UN, umekuwa chanzo cha maendeleo, ushirikiano, umoja na ulinzi wa amani na haki za binadamu duniani.

Tumeona mambo mengi na mafanikio duniani yakipatikana kupitia mkono wa Umoja wa Mataifa. Kwa miaka mingi umekuwa rafiki wa Afrika, ukisaidia kuleta mipango na mikakati mbalimbali pamoja na rasilimali za kuondoa umaskini.

Tunashuhudia mashirika yake kama lile la watoto –UNICEF likihimiza, kusimamia na kusaidia kwa hali na mali maisha bora na afya endelevu ya watoto wetu kuanzia chanjo na hata dawa muhimu.

Si hivyo, tu jumuiko hilo, limewezesha kupambana na vifo vya wajawazito, wazazi na watoto kupitia miradi mbalimbali ya afya iliyokuwa inaainishwa kwenye programu ikiwamo ya maendeleo ya milenia.

Aidha, UN kupitia Shirika la Afya WHO imekuwa mstari wa mbele kupambana na maradhi yanayotishia dunia na hasa Afrika ili kuendeleza ustawi wa watu, afya  na maisha bora.

Kwa sasa hakuna anayepingana na  kazi kubwa inayofanywa na WHO kupambana na kudhibiti kitisho cha ebola Afrika na kuzuia maangamizi makubwa ambayo yangetokea iwapo ugonjwa huo usingedhibitiwa kwa jitihada hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, anapozungumza katika maadhimisho ya kuzaliwa UN anasema Tanzania imejipanga kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ya UN kwa kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Anapozungumza huko Dodoma kwenye kusherehekea siku ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa  inayoongozwa na  kauli mbiu ‘Wanawake na Wasichana katika mstari wa mbele kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG)’.

Anawahakikishia wadau na UN kuwa  serikali imewekeza kwenye miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), barabara, bandari, viwanja vya ndege na bwawa la kufua umeme Rufiji ili kuwa na uwezo wa kiuchumi wa kutoa huduma kwa wananchi wake.

Anakumbusha kuwa uwekezaji mkubwa kama huo hauwezi kutenganishwa na  miradi  ya maendeleo ya kijamii kama kutoa elimu bure, huduma za afya, maji safi na salama pamoja na kuimarisha uchumi.

Kwa vile jambo kubwa la UN kwenye maadhimisho hayo ni usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake kwenye maendeleo endelevu, Tanzania haina budi kulitekeleza kwa vitendo.

Waziri wa Mambo ya Nje, anapozungumzia suala la ukatili wa kijinsia anasema ni lazima kuukomesha ukatili huo na taifa linatoa kipaumbele.

Anasema kuna mkakati wa kuleta usawa wa kijinsia ambao baadhi ya mambo yanayofanyika hata sisi tunayashuhudia.

Mojawapo ni Rais John Magufuli, kusimamia kwa dhati na kuwataka viongozi wa serikali kuanzia wabunge, polisi, wanasheria, wakuu wa mikoa na wilaya kumaliza suala la mimba za utotoni na ndoa za mabinti.

Aidha, pamoja na kutaka suala hilo kutokomezwa serikali inasimamia utoaji wa mikopo ya riba nafuu kwa vijana, kinamama na walemavu ili wawekeze na kuanzisha miradi ya maendeleo.

Tunaomba hatua zichukuliwe zaidi kuimarisha ustawi wa wanawake na mabinti lengo likiwa ni  kutimiza azma ya UN kupitia kauli mbiu ‘Wanawake na Wasichana katika mstari wa mbele kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG)’.

Tunaamini kukomeshwa ukatili dhidi ya wanyonge hawa, kuboresha huduma za uzazi salama, kupewa nyenzo na mitaji ya uwekezaji, kupata elimu na kushirikishwa kwenye nafasi za uongozi wa kisiasa, kijamii, kiuchumi wanawake wa Tanzania watakuwa na nafasi nzuri ya maendeleo endelevu.

Tunapoungana na UN kusherehekea kutimiza miaka 74 tunaona kuwa kipaumbele chetu kiwe maendeleo endelevu kwa wote ili tuwe na Tanzania yenye amani na furaha kwa raia wote.

Habari Kubwa