Yanga ikitekeleza haya  Pyramids itafia Kirumba

26Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Yanga ikitekeleza haya  Pyramids itafia Kirumba

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Yanga watashuka dimbani kesho kwenye mechi ya kwanza ya mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Yanga imeangukia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Zesco ya Zambia kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo kesho itaikaribisha Pyramids ya Misri katika Uwanja wa CCM Kirumba kusaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe hilo la Shirikisho.

Na ili Yanga iweze kufuzu hatua hiyo, itahitaji kupata matokeo ya jumla katika mechi mbili, ya kesho na zitakaporudiana wiki mbili zijazo nchini Misri.

Tayari Pyramids wamewasili nchini kwa ajili mechi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa ngumu kwa timu zote, lakini Yanga ikitarajiwa kutumia vema uwanja wake wa nyumbani kabla ya kuwafuata Wamisri hao kwao.

Tunatambua Pyramids ambayo kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Misri ikiwa na alama 11 baada ya kushuka dimbani mara tano mechi moja mbele dhidi ya Zamalek yenye pointi 10 katika nafasi ya pili, si timu ya kubeza hata kidogo na inaundwa na nyota wengi kutoka Amerika Kusini.

Miongoni mwa wachezaji nyota wanaounda kikosi cha Pyramids ni pamoja na nyota kutoka Brazil na Colombia ambao gharama ya kuwanunua inaelezwa kuwa zaidi ya Sh. bilioni 70 za Tanzania, jambo linaloashirikia ni wa daraja la juu.

Hata hivyo, Nipashe tunaamini gharama ya mchezaji haiwezi kuwa sababu kwa Yanga kuihofia Pyramids katika mechi hiyo ya kesho itakayoamua hatima yao kwenye michuano ya kimataifa baada ya wawakilishi wengine wa Tanzania, Simba, Azam, KMC, KMKM na Malindi kutolewa katika kinyang'anyiro hicho.

Ni kweli tunakubaliana na gharama ya mchezaji mara nyingi inatokana na ubora wake, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kujiaminisha kuwa inaweza kuibeba Pyramids mbele ya Yanga ambayo itakuwa katika uwanja wake wa nyumbani ikiungwa mkono na mashabiki wake.

Tulishuhudia msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ikiwazima ndugu wa Pyramids, Al Ahly ya Misri katika Uwanja wa Taifa kwa bao 1-0, wakati wengi wakiamini wawakilishi hao wa Tanzania wangeangukia tena pua baada kuchezea kichapo cha mabao 5-0 ugenini.

Wengi walijiamisha kuwa Simba ingechezea tena kichapo nyumbani na imani hiyo ikiongezeka kutokana na Al Ahly kuundwa na wachezaji bora na ghali ambao mmoja tu gharama yake ilikuwa ni mara tano zaidi ya bajeti ya kikosi kizima cha Wekundu wa Msimbazi hao.

Hivyo kwa maandalizi ambayo Yanga imefanya ikiwa ni pamoja na kuwavuruga wapinzani wao kisaikolojia kwa kuwapeleka Uwanja wa CCM Kirumba hatua iliyozua hofu kwao kuwa wanapelekwa 'machinjoni' kunaweza kuwapa wawakilishi wetu hao matokeo mazuri.

Kinachotakiwa kwa Yanga si tu kupata matokeo bali pia kuhakikisha inapata ushindi wa kishindo huku ikiepuka kutoruhusu bao la ugenini kwa wapinzani wao ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele watakaporudiana wiki mbili zijazo nchini Misri.

Nipashe tunaikumbusha Yanga kuwa makini na mashambulizi ya kushtukiza na kucheza mchezo wa kasi mwanzo mwisho kwani falsafa za timu za Kiarabu mara nyingi ni kucheza taratibu na kushambulia kwa kushtukiza huku wakipoteza muda mwingi wakiwa ugenini.

Lakini pia mashabiki wa Yanga na Watazania kwa ujumla, hawana budi kuitumia vema nafasi yao ya kuwa mchezaji wa 12 timu inapocheza nyumbani kwa kuishangilia mwanzo mwisho huko wakiwaozomea wachezaji wa Pyramids kila wanapogusa mpira.

Tunataka kuona Yanga ikisonga mbele ili kutetea nafasi ya Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, hivyo hili si jukumu la wawakilishi hao tu, bali Watanzania wote hawana budi kuungana katika kuhakikisha Yanga inasonga mbele katika michuano hiyo ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa.

Habari Kubwa