Ndayiragije aachwe huru Stars akipewa ushirikiano 

28Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Ndayiragije aachwe huru Stars akipewa ushirikiano 

HATIMAYE Shirikisho la Soka nchini (TFF), limehitimisha mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars kwa kumrasimisha Mrundi Etienne Ndayiragije aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo. 

Ndayiragije sasa amechukua rasmi mikoba ya Mnigeria Emmanuel Amunike aliyefungashiwa virago vyake baada ya matokeo mabaya ya Stars kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Misri mwaka huu.

Aidha, Ndayiragije ambaye wakati akikaimu nafasi hiyo alikuwa akisaidiwa na Kocha wa Polisi Tanzania, Selemani Matola pamoja na Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda, amekabidhiwa mikoba hiyo tayari akiwa ameipa Stars mafanikio. 

Kocha huyo wa zamani wa KMC na Azam FC, ameiwezesha Taifa Stars kucheza hatua ya makundi kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022. Si mafanikio hayo tu, bali pia ameiongoza Taifa Stars kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zitakazofanyika nchini Cameroon Aprili mwakani.

Hakika Ndayiragije anaanza majukumu hayo rasmi akiwa na mafanikio makubwa, hivyo anahitaji kupewa ushirikiano mkubwa ili kuweza kuendelea kuwapa raha Watanzania kwa kuifikisha Stars mbali zaidi.

Tunauhakika Ndayiragije anaweza kufanya makubwa zaidi kama ataachwa afanye kazi yake akiwa huru pasi kuingiliwa katika majukumu yake wala kuwapo kwa shinikizo lolote kwake wakati wa kuchagua wachezaji wa Stars ama kupanga kikosi chake.

Tunatambua kuwapo kwa utamaduni kama huo ama kutoka kwa viongozi wa TFF au wa klabu kongwe, lakini kutokana na kelele za wadau wa soka kama si mashabiki husika wa klabu hizo.

Lakini pia, Nipashe hatuna budi kumsisitiza Ndayiragije katika kutekeleza majukumu yake hayo azingatie zaidi ubora na viwango vya wachezaji na asitekwe na nguvu kubwa za U-simba na U-yanga.

Kwa miaka kadhaa sasa tumekuwa tukishuhudia makocha wa Taifa Stars wakitekwa na U-simba na U-yanga hivyo kulazimika kutafuta uwiano wa wachezaji kutoka klabu hizo wakati wa kutangaza kikosi cha timu ya taifa.

Tunaamini kama ambavyo Ndayiragije katika mechi ya marudiano ugenini dhidi ya Sudan kuwania kufuzu CHAN, alivyofanya kwa kutompanga mchezaji hata mmoja wa Yanga na Stars ikashinda 2-1 ataendelea kuzingatia viwango na si ukubwa wa klabu mchezaji anapotoka. 

Si kwa Yanga tu, lakini pia tumeshuhudia kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula akipoteza nafasi Stars dhidi ya Juma Kaseja wa KMC ambaye anasaidiwa na Metacha Mnacha wa Yanga. 

Nipashe tunataka kuona mchezaji wa Simba ama Yanga na klabu nyinginezo anapata nafasi Taifa Stars kutokana na ubora na kiwango chake tu na si kuongozwa na ukubwa ama ukongwe wa klabu anayoichezea au kutafuta uwiano kutoka timu hizo. 

Na hayo yote yatawezekana tu kama ambavyo TFF ya Rais Wallace Karia ilivyomwacha Ndayiragije kuamua mwenyewe wachezaji anaowataka na kutomwingilia katika upangaji wa kikosi chake.

Tunaamini huo ni mwanzo mzuri kwa Ndayiragije na sasa atakuwa na wigo mpana zaidi wa kuzunguka kila kona nchini kushuhudia mechi za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza kusaka wachezaji wenye sifa ya kuunda kikosi chake.

Nipashe tunamtakia kila la kheri Ndayiragije katika kutekeleza majukumu yake hayo, huku pia tukiwaonya wale wote wenye tabia ya kuingilia majukumu ya makocha wa Taifa Stars sasa kuacha mara moja tabia hiyo.

Habari Kubwa