Watumishi waliopanda kulipwa mishahara mipya

29Oct 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Watumishi waliopanda kulipwa mishahara mipya

SERIKALI imezitaka wizara na taasisi zote kuhakikisha zinawalipa mishahara pamoja na stahili zote watumishi ambao wamepandishwa madaraja kulingana na nafasi walizo nazo sasa kwa mujibu wa miongozo iliyopo ya utumishi wa Umma.

Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika

Agizo hilo lilitolewa jana jiji hapa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika, alipokuwa akizindua na kufungua mkutano wa Baraza Kuu la Nne la wafanyakazi katika utumishi wa Umma.

Mkuchika alisema  kumekuwa na malalamiko katika maeneo mbalimbali nchini kuwa watumishi ambao serikali ilitoa maagizo kuwa wapandishwe madaraja mishara yao imebaki kama ilivyokuwa awali.

“Hivi karibuni nilikuwa mkoani Ruvuma huko pia nimekutana na malalamiko ya kutosha, kila mtumishi analalamika kuwa kapanda daraja, lakini mshahara bado haujapanda,” alisema Mkuchika.

Alisema kutokana na hali hiyo viongozi wa serikali wanaohusika na suala hilo wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanalifanyia kazi ili  kuwapatia stahili zao watumishi wote waliopanda madaraja.

Pia aliagiza katika upandishaji wa madaraja kwa watumishi wapewe nafasi ya upendeleo wale ambao wanakaribia kustaafu.

“Serikali ilitangaza upandishaji wa madaraja kwa  wenye sifa, lakini pia wanaotakiwa kupatiwa kipaumbele ni wale ambao wanakaribia kustaafu katika utumishi wa Umma ili waweze kupata stahiki ambazo zitawawezesha kujikimu kule wanakokwenda,” alisema Mkuchika.

Alisema Novemba 1, mwaka 2017 serikali iliidhinisha watumishi wapatao 85,000 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka 2015/16 kupandishwa vyeo.

“Aidha awamu nyingine ya upandishaji wa vyeo imefanyika Mei 1, 2019 ambapo watumishi 193,166 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka 2017/18 wamepandishwa vyeo,” alifafanua Waziri Mkuchika.

Mkuchika pia aliwapongeza watumishi wote wa Umma ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kukusanya na kusimamia mapato ya serikali ambayo yanatumika katika kuboresha miundombinu mbalimbali.

“Niwapongeze sana watumishi kwani nyie ndiyo mmekuwa mkikusanya haya mapato ya serikali kwa kiasi kirefu kwani hapo zamani kabla ya hii awamu ya tano tulikuwa tukikusanya kwa mwezi kiasi cha Sh. bilioni 800, lakini sasa imefikia hadi Sh. trioni 1.7 kwa mwezi kiasi ambacho tunatakiwa kushikilia hapo hapo,”alisema

Vilevile, Mkuchika aliwataka watumishi wa Umma waliopo chini ya Ofisi ya Rais Utumishi na utawala Bora, kuhakikisha wanakuwa wa mfano katika suala la kupinga rushwa na kufanya kazi kwa uadilifu bila ya kuchagua maeneo ya kwenda kufanya kazi.

“Rushwa katika ofisi za Umma imekuwa kikwazo kwa wananchi wetu tunaowatumikia… naomba katika ofisi yangu watumishi wangu muwe watu wa mfano ambao mtakuwa hamjihusishi na rushwa hata kidogo ili kuakisi jina la utawala bora,“ alisema.

Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Leah Ulaya, alisema  moja kati ya changamoto ambazo zimekuwa kero kwa watumishi ni upandishwaji wa madaraja bila kuzingatia stahiki nyingine ikiwamo mishahara.

“Tunakuomba mheshimiwa waziri suala hili lifanyiwe kazi ili sisi watumishi ambao tumepata fursa ya kupanda madaraja tuweze kupata stahiki zetu kulingana na miongozo ya utumishi wa Umma,” alisema Ulaya.

Habari Kubwa