Sababu vijana kupata kiharusi kwa kasi 

29Oct 2019
Romana Mallya
Nipashe
Sababu vijana kupata kiharusi kwa kasi 

MATUMIZI ya sigara, pombe, uzito kupita kiasi, kula bila mpangilio umechangia vijana wenye umri wa miaka 30 kuendelea kupata kiharusi.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ubongo, Mishipa ya Fahamu na Uti wa Mgongo upande wa Upasuaji, Mugisha Clement, kutoka Hospitali ya Aga Khan, aliyasema hayo juzi na kueleza umri wa watu kupata kiharusi umeshuka na sasa kijana mwenye miaka 30 yupo kwenye hatari hiyo.

Akizungumza na Nipashe  ikiwa ni Siku ya Ugonjwa wa Kiharusi Duniani, Dk. Clement alisema awali kundi la watu waliokuwa kwenye hatari ya kupata kiharusi lilikuwa  ni kwa wale waliokuwa na umri kuanzia miaka 50 kuendelea, lakini sasa vijana wenye umri wa miaka 30 kuendelea wapo kwenye hatari hiyo.

"Vijana wapo kwenye hatari ya kupata kiharusi kwa sababu wengi wanavuta sigara, wanakunywa pombe, wanakula chakula kupita kiasi na bila mpangilio, wana uzito mkubwa na wanatumia dawa zinazohatarisha maisha yao.

"Vyote vinasababisha mtu kupata shinikizo la damu, ukiwa na shinikizo la damu katika umri mdogo kunauwezekano wa kupata kiharusi."

Dk. Clement alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kati ya watu wanne, mmoja atapata kiharusi.

Alisema mazoezi ni dawa na kuwashauri watu kwa wiki angalau wayafanye mara mbili au tatu.

Alitaja viashiria vya kiharusi kuwa ni mtu kuwa na uzito mkubwa na kutaka watu wapunguze wanga na waongeze matumizi ya mboga za majani.

"Vijana wengi  wanavitambi na hii ni moja ya hatari ya kupata kiharusi kwa sababu mwili unakuwa na mafuta mengi kwenye damu ambayo hujiweka kwenye kuta za mishipa ya damu kwa hiyo utapata shinikizo la damu mwisho wa siku itapasuka," alisema.

Vilevile alisema kwa wanaotumia sigara husababisha uharibifu kwenye kuta za mishipa ya damu na kuifanya ikakamae.

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mishipa ya Ubongo, kutoka hospitali hiyo, Philip Adebayo, alisema zipo aina mbili za kiharusi ambazo ni mishipa kuziba na damu kushindwa kupita kama kawaida na ya pili ni mishipa ya kupitisha damu kupasuka.

"Kila mtu yupo hatarini kupata kiharusi, tuitunze miili yetu, tufanye mazoezi kwa sababu matukio ya ugonjwa wa kiharusi yanaongezeka hasa nchi zinazoendelea," alisema.

Habari Kubwa