DC azuia uchomaji wa nyumba za wananchi

29Oct 2019
Gurian Adolf
NKASI
Nipashe
DC azuia uchomaji wa nyumba za wananchi

MKUU wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda, amepiga marufuku kitendo cha askari wa Pori la Akiba Lwafi, kuchoma moto nyumba za wakazi wa kijiji cha Mpata Kata ya Kirando kisha kuwaondoa kwa nguvu kwa madai wanaishi ndani ya hifadhi.

Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda

Marufuku hiyo imetokana na askari hao kuvamia kijiji hicho na kuendesha operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu wananchi hao pamoja na kuchoma moto nyumba zao, huku wakitoa siku tatu wakazi wengine wa kijiji hicho wawe wamehama.

Akizungumza  na wananchi hao baada ya kupokea malalamiko yao, alisema amesitisha operesheni ya kuwaondoa na ameunda timu maalumu ya wataalamu wakiwamo maofisa ardhi watakaokwenda kupima eneo hilo ili kubaini mipaka kati ya kijiji na pori la akiba.

Alisema  baada ya timu hiyo kuwasilisha ripoti ndipo serikali itabaini ukweli iwapo kijiji hicho kipo ndani ya hifadhi au sivyo, na kama kijiji hicho kipo ndani ya hifadhi, utaandaliwa utaratibu wa kuwaondoa.

Aliwataka wananchi hao kuendelee kuishi katika kijiji hicho bila kubugudhiwa na mtu yeyote hadi timu itakamilisha kazi yake na kuwa serikali itatoa taarifa kwao.

''Lengo la serikali ni kuona hakuna mtu anayeonewa na kama jambo hilo limefanyika, basi halitaendelea tena na kila mmoja atapata haki yake kulingana na taarifa ya timu itakavyobainisha ukweli wa jambo hilo,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa kijiji hicho, Raymond Makanta, alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa wananchi wanaishi kwa taabu na kwa wasiwasi baada ya askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kuvamia kijiji hicho na kuwa wanahitaji msaada wa haraka kwa kuwa mali zao zimeharibiwa na  wamepewa siku tatu wawe wameondoka kijijini hapo.

Diwani wa Kirando, Kakuli Seba, alimshukuru mkuu wa wilaya kwa kufika kwa wakati katika eneo hilo kwani amani ilikuwa imetoweka na kueleza kuwa kitendo cha kuwazuia askari hao kuendelea na operesheni  inaonyesha kuwa  serikali ipo kazini na inatatua kero za wananchi kwa wakati.

Alisema anaamini serikali italitafutia ufumbuzi wa haraka jambohilo ili wananchi waendelee kuishi kwa amani na furaha kama ilivyokuwa awali.

Habari Kubwa