Jafo atoa maagizo sita uchukuaji fomu

29Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Jafo atoa maagizo sita uchukuaji fomu

UCHUKUAJI na urejeshaji fomu kwa ajili ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, unaanza leo, huku serikali ikitoa maagizo sita kuhusu uzingatiaji kanuni katika mchakato huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo,

Uchaguzi huo utafanyika Novemba 24, mwaka huu na nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti wa Kitongoji, katika Mamlaka za Miji Midogo, Mwenyekiti wa Mtaa na wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi mchanganyiko la wanawake na wanaume) na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (kundi la wanawake) katika Mamlaka za Miji.

Nyingine ni Mwenyekiti wa Kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi mchanganyiko la wanawake na wanaume), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi la wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema uchukuaji na urejeshaji wa fomu utafanyika kwa siku saba ambao utaanza leo hadi Novemba 4, mwaka huu.

Alieleza kuwa fomu hizo zinapatikana kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwenye ofisi za watendaji wa vijiji na mitaa. 

Kutokuwa na muingiliano

Aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha utoaji fomu hauingiliani na changamoto ya aina yeyote kama walivyopewa maelekezo.

“Watanzania wenye nia ya kushika nafasi mbalimbali kwenye mamlaka za serikali za mitaa huu ni muda mwafaka wa kufanya hivyo kupitia vyama vyao vya siasa vyenye usajili wa kudumu, ni kipindi muhimu watu wazingatie kanuni,”alisema.

Aliwasisitiza kusimamia kanuni katika mchakato mzima wa kuchukua na kurejesha fomu.Kusimamia demokrasia

Aidha, Jafo aliwataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake stahili ya kidemokrasia kama ambavyo serikali inakusudia.

“Kumekuwapo na utulivu kila mahali, watu wanaotaka ufafanuzi… wamekuwa wakituma barua na tunatoa ufafanuzi, lengo letu ni kuhakikisha kila mtu anashiriki katika uchaguzi huu bila kukwazwa na jambo lolote,” alisema. 

Waziri huyo alisema serikali inataka kuona kila Mtanzania anapata haki yake ya msingi ya kutimiza matakwa ya kidemokrasia.

Marufuku kampeni kabla 

“Kampeni kabla ya uchaguzi hairuhusiwi, naamini hata watu wakileta mbwembwe za aina yeyote, lakini zisiwe katika ‘style’ ya kampeni kwenye uchukuaji fomu, huwezi kumzuia kuchukua fomu kwa namna anayotaka,” alisema.

Aliongeza: “Mtu kusindikizwa na rafiki zake kwenye kanuni halijawekwa, lakini jambo hilo linapaswa lisiwe kampeni.”

Agizo kwa Ma-RC, Ma-DC

Jafo aliwaagiza Wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha maeneo yanakuwa tulivu na watu watimize matakwa ya kidemokrasia.

Vyama vyaonywa

Alivitaka vyama vya siasa kuhakikisha vinatumia vizuri demokrasia kwa kupeleka watu wanaowakusudia na kuwadhamini kwa mujibu wa kanuni.

“Hatutarajii itokee changamoto ya aina yeyote na kama kuna jambo halijaeleweka vizuri, watu waliweza kuomba ufafanuzi na nimetoa ufafanuzi kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu na namna ya kuchukua na kurejesha fomu,” alisema.

Alieleza kuwa anaamini ufafanuzi huo utakuwa umesaidia ili kushiriki vizuri katika mchakato huo kwa siku saba.

Katazo kwa watendaji 

Alisema kutokana na uongozi kukoma kwenye nafasi hizo Oktoba 22, mwaka huu shughuli zote zipo chini ya watendaji wa vijiji na mitaa na zitaendeshwa kwa mujibu wa sheria na watashirikiana na watendaji wa kata husika.

“Agizo kwa watendaji wa vijiji na mitaa hawataruhusiwa kutekeleza jukumu lolote ambalo linapaswa kuamuliwa kwanza na Halmashauri za vijiji au mitaa,” alisema.

Alifafanua kuwa kuna majukumu ambayo yanapaswa kuamuriwa na Halmashauri za vijiji au mitaa, hayapaswi kufanywa na mtendaji wa kijiji na lazima yaende kwa mtendaji wa kata na kuwasilisha kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuangalia namna ya kulitatua.

TGNP yafunda wanawake

Wanawake wenye dhamana za uongozi wametakiwa kuongoza kwa hekima na malengo mazuri  yenye kuleta mafanikio, ili  wawe kumbukumbu nzuri itakayowavutia  vijana na vizazi vijavyo.  

Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Assey Muro, aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua mafunzo kwa wanawake zaidi ya 100 wa Dar es Salaam waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chaguzi wa  Serikali za mitaa jijini hapa.  

Muro alisema  wanawake wamekuwa ni viongozi wazuri kuanzia kwenye kaya, usimama katika kuhakikisha familia hazipotezi mwelekeo bali zinapiga hatua za kimaendeleo, hivyo anaamini kuwa wanaopata uongozi wataendelea kuwa viongozi wazuri. 

“ Muwe mfano bora kwa vizazi vyetu, kijana akikaa awaze kuwa natamani kuwa kama akutaje jina kwa namna ulivyomvutia, sisi TGNP tuko pamoja katika kuhakikisha mnavuka na kufanikisha malengo  ya maendeleo yaliyowekwa,” alisema Muro. 

Alisema wajitahidi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutafuta njia ya kutatua kero zinazowakabili  jamii wanapoishi, kama vile kukosekana kwa maji safi na salama, huduma bora za afya na elimu. 

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Hilda Dadu, alisema malengo ya TGNP ni  kuwajenga wagombea uelewa wa mchakato ya uchaguzi ushiriki wa wanawake na kuweka mbinu za ushindi. 

Alisema pia kupitia mafunzo hayo wanalenga kuwajenga uwezo wagombea kutambua jinsi ya kujenga ajenda za vipaumbele vitakavyowawezesha wakubalike. Kuweka mkakati wa pamoja ya kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kubeba agenda ya wanawake wakati wa uchaguzi na baada. 

Katika Ilani ya Uchaguzi ya wanawake, uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na uchaguzi Mkuu mwaka 2020 ambayo wanawake hao walipewa  kuna madai kadhaa ikiwamo kuhoji vyama vya siasa kuwa na mapengo ya jinsia ndani ya uongozi wa vyama. 

Pia vimetakiwa kuzingatia idadi ya wagombea wote nafasi za ushiriki wa wanawake isipungue asilimia 50, pia viweke mikakati ya kuwezesha wanawake na makundi maalum kwenye kampeni.  

Ilani hiyo iliyobeba ajenda ya Mwanamke, Turufu ya Ushindi mwaka 2019/2020 imeandaliwa na taasisi tatu ambazo ni pamoja na TGNP Mtandao, Mtandao wa Wanawake na Katika   na Women Fund Tanzania. 

Ilani hiyo inabainishwa kuwa  imelenga kuhamasisha wanawake, wapigakura kukataa kuendelea kutumia kama wapiga debe, wasindikizaji, waburudishaji  katika kampeni na waathirika  wa umasikini. 

 

Imeandikwa na Agusta Njoji, Dodoma na Beatrice Moses, Dar 

Habari Kubwa