Mabalozi wapya watangaza neema 

29Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam.
Nipashe
Mabalozi wapya watangaza neema 

RAIS John Magufuli jana alipokea hati za utambulisho za mabalozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Manfred Fanti, wa Finland, Riitta Swan na wa Rwanda nchini, Meja Jenerali Charles Karamba, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza baada ya kuwasilisha hati zao kwa nyakati tofauti, mabalozi hao wapya walitoa kauli za matumaini na manufaa kwa nchi zao na Tanzania.  

Akizungumza baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho, Balozi Fanti aliishukuru Tanzania kwa kumpokea kuiwakilisha EU nchini na kwamba katika kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na EU na Tanzania, atajielekeza zaidi katika masuala ya maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Balozi Fanti anaamini kuna mambo mengi na mazuri ya kufanya yatakayoiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kama ilivyopanga.

Aliongeza kuwa anaamini katika mazungumzo ya pamoja kati ya Tanzania na EU katika masuala mbalimbali na kwamba katika kipindi chake anatarajia kutilia mkazo miradi ya kuzalisha nishati ya umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na utekelezaji wa miradi mingine iliyoko katika makubaliano ya 11 ya mkataba wa mfuko wa maendeleo wa EU uliotengewa Sh. trilioni 1.583.

Rais Magufuli alimpongeza mwakilishi huyo kwa msimamo wake wa kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na EU. 

Alisema Tanzania inatambua uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na EU na kwamba iko tayari kushirikiana na balozi huyo katika utekelezaji wa masuala yenye maslahi kwa pande zote mbili.

Naye Balozi Swan pamoja na kushukuru kwa kupokewa,  alimpongeza Rais Magufuli kwa mafanikio makubwa katika kupambana na rushwa na akasema katika kipindi chake nchini atahakikisha maeneo ya uhusiano kati ya Tanzania na Finland yanaimarishwa ikiwamo mradi wa utunzaji wa mazingira, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na utawala bora.

Rais Magufuli, kwa mujibu wa taarifa hiyo, alimshukuru kwa dhamira yake ya kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano na Tanzania na kwamba Tanzania itakuwa tayari kutoa ushirikiano wowote atakaouhitaji.

Kwa upande wake, Jenerali Karamba, taarifa hiyo ilisema, aliishukuru Tanzania kwa kumkaribisha na kumhakikishia Rais Magufuli kuwa katika kipindi chake  atahakikisha matarajio ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ya  kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Rwanda yanafanikiwa.

 Rais Magufuli alimkaribisha  Balozi Karamba na kumtaka ahakikishe biashara kati ya Tanzania na Rwanda inakuwa zaidi ikiwamo kutekelezwa kwa makubaliano yake na  Rais Kagame wa Rwanda kutumia Bandari ya Tanga katika upokeaji na usafirishaji wa mizigo ya kwenda na kutoka Rwanda.

“Sisi ni ndugu na ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwenyekiti wetu ni Rais Kagame. Hatuna sababu ya kupoteza muda, nataka usukume sana suala la kuongeza biashara kati ya Tanzania na Rwanda ili nchi zetu zinufaike zaidi,” alisisitiza Rais Magufuli.

Habari Kubwa