Ndivyo tunavyoanza uchaguzi wa mitaa

29Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Ndivyo tunavyoanza uchaguzi wa mitaa

MCHAKATO wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaanza rasmi leo. Na huu ndiyo wakati wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi uwe katika serikali za vitongoji, vijiji na mitaa leo ndiyo siku muhimu ya kuanza kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya uchaguzi huo unaofanyika mwishoni mwa mwezi ujao.

Tukumbuke kuwa uchaguzi huo utafanyika Novemba 24 na nafasi zitakazojazwa ni wenyeviti wa vitongoji, mitaa na wajumbe wa kamati ya mtaa, wenyeviti wa vijiji pamoja na wajumbe wa halmshauri  za vijiji.

Kwa hiyo kuanzia sasa  tunawakumbusha wagombea kuwa wana siku saba za kuchukua na kurejesha fomu hizo ambazo siku ya mwisho wa kuzirudisha ni Novemba 4, 2019.

Fomu hizo zinatakiwa kujazwa na kuwekewa taarifa zote za msingi za mgombea ambaye pamoja na mambo mengine usahihi ni jambo la kuzingatia.

Kwa ujumla tunapenda kuona uchaguzi huu wa ngazi za chini au kwenye mashina unaowahusu wananchi wetu, ukifanyika kwa amani na utulivu, usawa, maridhiano na zaidi kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia.

Mara nyingi kwenye mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu ndiko kunakokuwa na mizengwe. Kuna madai kuwa mara nyingi wagombea wakirudisha fomu, maofisa wanaotakiwa kupokea fomu hizo hasa siku ya mwisho huingia mitini na wagombea wanapofika wanakuta ofisi zimefungwa.

Yote hayo yanadaiwa kufanyika ili kukwamisha baadhi ya wagombea kwa maelezo kuwa fomu zao hazikufikishwa kwa wakati.

Tunaomba wahusika wafanyekazi hizo kwa uadilifu na kwa haki kwa vile kila mshiriki ana haki kikatiba ya kuchagua na kugombea ili achaguliwe kuwa kiongozi ama awachague viongozi anaowapenda.

Tungependa kusisitiza kuwa mizengwe na udanganyifu si jambo jema wakati huu ambao watu wengi wanautizama uchaguzi wa serikali za mitaa kama hatua ya kwanza yakuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2020.

Aidha, tunavikumbusha vyama kuwapa nafasi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki kwa kuwapa maeneo ya  kugombea kwani kuna nyadhifa mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa huu ni uchaguzi mkubwa kwani takribani viongozi 1,000,000 wanachaguliwa nchini kote, hili si jambo la kuupuuzwa.

Ndiyo maana tunawasihi wasimamizi wa uchaguzi wanaoshughulikia kupokea fomu wawe watenda haki,  wakati mwingine suala la kuweka mapingamizi limekuwa  likifanywa pengine kwa nia ya kuharibiana.

Tungependa kusema hakuna sababu ya kuharibiana kwa kuzua na kutangaza ubaya usio na sababu dhidi ya mgombea kwa nia ya kuvuruga demokrasia.

Ni vizuri kila Mtanzania akapata haki yake ya msingi ya kutimiza matakwa ya kidemokrasia na kufanya kila jambo kwa hatua kama ambavyo serikali inaelekeza.

Wagombea wakumbuke kuwa kampeni wakati wa kuchukua fomu haziruhusiwi, licha ya kwamba wanaweza kuchukua fomu kwa namna wanavyotaka, lakini si kuleta mbwembwe zinazoashiria kufanya kampeni.

Kwa upande wa vyama huu ndiyo wakati wa kutumia wanachama wenye sifa ili kuondoa mafarakano ndani ya chama.

Tunavikumbusha vyama kuwa ni jukumu lake kuwadhamini kama ambavyo  kanuni zinavyoelekeza.

Nasi tunaungana na maelezo ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayesema kuwa serikali haitarajii itokee changamoto ya aina yoyote kubwa ya kuvuruga uchaguzi.

Endapo kutatokea jambo lisiloeleweka wagombea na watu wengine waliulize kwa mamlaka za kusimamia uchaguzi.

Habari Kubwa