Serikali isimamie maelekezo ili wakulima wa pamba walipwe

29Oct 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Serikali isimamie maelekezo ili wakulima wa pamba walipwe

KUNA maelezo mengi yanayoweza kutolewa kuhusu kadhia ya wakulima walio wengi wa pamba kutolipwa fedha zao hadi sasa, tangu msimu wa pamba ulipozinduliwa Mei 2, mwaka huu mkoani Katavi.

Hiyo ni pamoja na ukweli kwamba pamba waliyoiuza kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), imeshasafirishwa na matajiri kutoka kwenye maghala ya vyama hivyo, bila ya kuwalipa stahiki yao.

Hata hivyo, lililo la msingi ambalo Muungwana analiona ni la kulipwa kwa fedha hizo za wakulima hawa ambao wengi wao ni wadogo wadogo, wakiendesha maisha kwa kulitegemea zao hili hususan katika maeneo linakolimwa.

Nasema hili ni la msingi zaidi kwa sababu maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na serikali kwa nyakati tofauti kuhusiana na kadhia hii, bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu na wanunuzi wa zao hilo.

Na matokeo yake ni haya yanayoripotiwa kutoka maeneo mbalimbali, jinsi wakulima wanavyohangaikia kupata fedha hizo kwa miezi sasa.

Kwa muda wote wa takribani miezi sita iliyopita, Muungwana amekuwa akieleza jinsi hatua ya kutolipwa kwa fedha hizo inavyozidi kuwadidimiza wakulima hawa kimaisha na kukwamisha mipango yao ya kuongeza tija katika kilimo.

Muungwana anasema hivyo kwa sababu wakulima ambao pamba ni zao la biashara, wanalitegemea kama chanzo chao kikuu cha kuwaingizia mapato ambayo pamoja na mengine huyatumia kugharimia maandalizi ya mashamba, pembejeo na mahitaji mengine.

Lakini mapato hayo hutumika kwa minajili ya manunuzi ya chakula, ikichukuliwa ukweli kwamba baadhi ya maeneo ya mikoa kunakolimwa pamba hayakupata chakula cha kutosha msimu uliopita.

Kwa hali hiyo wanategemea fedha ya mauzo ya pamba ili wanunulie chakula, huku bei ya baadhi ya mazao ya vyakula kama mahindi sasa ikiwa imefikia kiasi cha 16,000/- kwa debe, kwenye maeneo yanayolima pamba kama zao la biashara.

Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa mfano fedha zitokanazo na mauzo ya pamba ndizo hutumika katika ununuzi wa mifugo kama ng’ombe, ujenzi wa nyumba bora, ununuzi wa vifaa vya usafiri kama baiskeli, bodaboda, bajaji, tela za kukokotwa na wanyama na raslimali zingine.

Aidha, wanategemea mapato ya zao hilo kwa ajili ya kununulia sare za watoto wao, ada na mahitaji mengine muhimu ya kimaendeleo.

Sasa haya yote kimsingi yamekwama na ndiyo maana hali si nzuri kwa wakulima hawa, wakati tayari katika maeneo yao msimu mpya wa kilimo umeshaanza na mvua zinaendelea kunyesha.

Kama nilivyosema, mengi yanaweza kuelezwa na kwa kweli yanaendelea kuelezwa na wanunuzi ambao kwa maoni ya Muungwana, wanakwamisha maendeleo ya wakulima hawa.

Wanunuzi wanadai kuporomoka kwa bei ya zao hilo katika soko la dunia kama sababu ya msingi ya wao kutowalipa fedha wakulima hawa pamoja na kwamba tayari wameshasafirisha pamba ya wakulima hawa kutoka AMCOS na kuipeleka kwenye viwanda vyao vya kuchambua pamba.

Kwa maana nyingine wanunuzi hawa ni kama vile wamewakopa wakulima, lakini kuwalipa watoto wa mjini wanasema, inakuwa ‘ngoma nzito.’

Taarifa ambazo Muungwana amekuwa akizipata kutoka kwa viongozi wa baadhi ya AMCOS ni kwamba kwa miezi sasa wamekuwa wakiahidiwa kupelekewa fedha na wanunuzi karibu kila siku lakini siku, wiki, na sasa miezi inakatika, hakuna kinachoendelea zaidi ya kuacha kilio kwa wakulima.

Hali iko hivi hata baada ya Rais John Magufuli kuwa ametoa siku 14 Oktoba 9, akiwa Katavi kwa wanunuzi kuhakikisha wanawalipa wakulima fedha zao ili kujiandaa na msimu mpya wa kilimo.

Bado ni rai basi ya Muungwana kwa serikali isimamie maelekezo yake ili wakulima wa zao hili ambao bado hawajalipwa waweze kulipwa fedha zao ili zistawishe maisha yao.

Habari Kubwa