Miss World 2019, Miss Tz wagawa taulo za kike, watoa elimu

29Oct 2019
Dotto Lameck
Arusha
Nipashe
Miss World 2019, Miss Tz wagawa taulo za kike, watoa elimu

MREMBO wa Dunia 'Miss World' 2019, Vanessa Ponce akishirikiana na Miss Tanzania 2019, Sylivia Sebastian, wametoa elimu ya hedhi salama na kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Moshono jijini Dar es Salaam.

Elimu hiyo imetolewa jana na walimbwende hao wakati wa kampeni ya kumsitiri mtoto wa kike na uzinduzi wa mashine ya kutengeneza taulo za kike ziitwazo Uhuru Pads, na kugawa taulo 1000 kwa wanafunzi hao. Huku Sebastian akionesha kufurahishwa kwa kushiriki kampeni hiyo ya kumsitiri mtoto wa kike na kusema kuwa jambo hilo limemgusa kwa kuwa limeshakuwa ni tatizo kwa watoto wengi wa kike.

“Wanafunzi wengi wamekuwa hawaendi shule katika kipindi cha hedhi kutokana na kuwa na wasiwasi, jambo ambalo limewapelekea kufeli masomo yao, hivyo tumeona tuje kutoa taulo hizi za kike ili matatizo haya yanayowakumba watoto wa kike yanaisha”. Amesema Sebastian.

Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe, amemshukuru Vanessa Ponce kwa kuitembelea nchi yetu na kuipongeza kamati nzima ya waandaaji wa Miss Tanzania kwa kumleta miss Vanessa ambaye ni Raia wa Mexico na kuanzisha kampeni huyo ya kugawa taulo za kike kwa wasichana wa shule za sekondari.

“Tumpongeze Rais wetu kwa kuzui matumizi ya mifuko ya plastiki kwani zuio hilo limepelekea hata wageni kuja na kutuletea taulo hizi za kike ambazo hazina mfuko wa plastiki kwani zinaoza na hata vifungashio vyake vinaoza”. Amesema Mwakyembe.

Mwakyembe amesema serikali itakuwa nao sambamba ili kuhakikisha wanafanikisha kampeni hii ya kumsitiri mtoto wa kike kwa kutafuta wadau wa kununua mashine kwa ajili ya kuzalisha taulo kwa lengo la kukidhi mahitaji ya watoto wa kike hapa nchini. 

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mashindano ya Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi, amesema hii ni bahati ya kipekee kwa mrembo anayeshikilia taji la urembo wa dunia kuja Tanzania tangu kuanzishwa kwa mashindano ya miss Tanzania mwaka 1994. 

Mwanukuzi alibainisha kuwa hivi karibuni Slyivia Sebastian anatarajiwa kuondoka kuelekea nchini uingereza kwenda kushiriki shindano la mrembo wa dunia ambalo fainali yake inatarajiwa kufanyika huko hivyo watanzania wajitaidi kumpigia kura ili aweze kushinda na hata wageni hawa waendelee kuona umuhimu wa kuja nchini Tanzania huku akitaja kauli mbiu ya mashindano haya kwa mwaka 2019 inasema urembo ni heshima hivyo kila miss Tanzania ambaye amewahi kushiriki shindano hili na anaetarajiwa kushiriki anatakiwa kutambua kauli hii na kuifanyia kazi.

kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Uhuru Sanitary pads Sara Gunda amesema kuwa wameamua kuwapa wasichana nafasi ili nao wajisikie kwamba kuna watu wanawajali katika swala zima la kuvunja ungo na itambulike kuwa uwezi kuwa mwanamke kamili kama ujavunja.

Aidha, amebainisha kuwa hadi sasa wameshatoa taulo za kike kwa wanafunzi elfu nne waliopo katika shule za sekondari za halmashauri ya wilaya ya Arumeru ,Monduli pamoja na jiji la Arusha na kusema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu  kwa wanafunzi wa kike katika shule zote za mkoa wa Arusha , Amesema lengo ni kuendelea kutengeneza na kugawa bure taulo hizo na ziweze kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wa kike na kuondoa changamoto walionayo

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Moshono, Neema Msuya, ameshukuru kwa ujio wa miss Dunia na kubainisha kuwa misaada waliopewa itawasaidia sana kwani kuna wanafunzi ambao wamekuwa hawaji shuleni pindi wanapokuwa katika kipindi cha hedhi kwani wengi wao wanaofia kuchafuka kitu kinachowasababishia kukosa masomo na kupelekea kufeli mitiani yao.

Habari Kubwa