Shughuli za kibinadamu zinaharibu Msitu wa Hifadhi ya Mporoto

29Oct 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Shughuli za kibinadamu zinaharibu Msitu wa Hifadhi ya Mporoto

Ofisa Utalii wa Hifadhi ya Mazingira Asilia ya mlima Rungwe, Jesca Mgata, ameeleza kuwa baadhi ya wananchi waishio kwenye vijiji vinavyouzunguka msitu wa Hifadhi wa Mporoto uliopo katikati ya Jiji la Mbeya na Wilaya ya Rungwe kuharibu mazingira ya msitu huo kwa kufanya shughuli za kibinadamu-

Baadhi ya watalii wa ndani kutoka mkoani Mbeya wakiangalia ziwa Ngosi ambalo linatajwa kuwa ni la pili kwa ukubwa barani Afrika kwa mabwawa yanayotokana na Volkano.

-hali ambayo inahatarisha ustawi wa msitu huo.

Mgata amesema hayo wakati wa ziara ya watalii wa ndani wakiwemo waandishi wa Habari na wasanii wa Mkoa wa Mbeya zaidi ya 20 ambapo walitembelea Ziwa Ngosi lililopo ndani ya msitu huo.

Amesema baadhi ya shughuli zinazofanywa na wananchi hao zinaharibu mazingira na kusababisha kubadilika kwa uhalisia wa msitu huo ambao ndio unasababisha Ziwa Ngosi ambalo halina mto unaoingiza maji wala unaotoa liendelee kuwepo.

Mgata amezitaja baadhi ya shughuli zinazofanywa na wananchi hao kuwa ni pamoja na uwindaji haramu, uchomaji moto hovyo hasa wakati wa kiangazi ambapo ndio kipindi wananchi hao wanaandaa mashamba kwa ajili ya kilimo, hivyo baadhi yao wanaingia hadi ndani ya msitu huo na kukata miti kama mianzi kwa ajili ya kujengea nyumba na kutengenezea nyundo pamoja na kuchingia mifugo

“Tunakabiliana na uharibifu huo wa mazingira kwa njia mbalimbali, tunatoa elimu ya utunzaji wa mazingira, tunawapatia ajira za muda hasa kutengeneza mipaka na kukwetua njia za kukabiliana na moto, tunawagawia mizinga ya nyuki na kuwagawia miche ya miti ili waipande kwa ajili ya kuni,” amesema Mgata.

amesema kutokana na umaarufu wa ziwa ngosi ambalo ni la pili kwa ukubwa barani afrika kwa maziwa yanayotokana na mlipuko wa volcano pamoja na umbo lake ambalo linafanana ramani ya bara la afrika idadi ya watalii imeanza kuongezeka na kufikia zaidi ya 700 kwa mwaka.

Aidha, amesema kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kuanza utekelezaji wa mpango wa kuiondoa mimea vamizi ndani ya Hifadhi ya misitu asilia ya Rungwe ukiwemo na msitu wa Mporoto.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Elimisha lenye Mkao yake jijini Mbeya ambalo linajishughulisha na mambo mbalimbali yakiwemo ya uhifadhi wa mazingira naupangaji wa bajeti, Festo Sikagonamo amesema, wananchi wanahitaji elimu ya kutosha ili watunze mazingira.

Amesema shirika lake linahusika na kuwaelimisha wananchi kupanga bajeti katika ngazi ya familia ili wapunguze hata matumizi ya nishati zitokanazo na miti ikiwemo mkaa na kuni hali ambayo alidai itasaidia kupunguza uharibifu wa misitu.

“Unakuta mtu mwingine ana mashamba matatu lakini mojawapo lipo kwenye chanzo cha maji, sasa sisi tunamfundisha namna ambavyo anaweza akayatumia mashamba mawili ambayo hayapo kwenye vyanzo vya maji na yakamletea mafanikio mazuri maana shida iliyopo ni kwamba wananchi hawapangi bajeti,” Amesema Sikagonamo.

Amesema msitu wa Mporoto ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya maji yanayotumika jijini Mbeya hivyo unahitajika kuhifadhiwa vizuri ili kuvilinda vyanzo hivyo.

Baadhi ya watalii waliotembelea Ziwa Ngosi, wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara zinazoenda kwenye ziwa hilo ili iwe rahisi kwa watalii kulifikia.

Naye mmoja wa wakilishi wa watalii hao wa ndani, Esther Mwakalobo, amesema ziwa hilo lina muonekano wa pekee na endapo miundombinu itaboreshwa watalii wengi watatembelea na kuliingizia Taifa mapato ya kutosha.

Habari Kubwa