Zahera aishukia Yanga kutimuliwa

30Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Zahera aishukia Yanga kutimuliwa
  • ***Asema alisajili kwa ajili ya Ligi Kuu na si kimataifa huku akidai Pyramids si saizi yao, Ally Mayay aionya klabu...

WAKATI mashabiki wa Yanga wakitaka Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera sasa atimuliwe huku uongozi wa timu hiyo, ukieleza umesikia "kilio" chao, na kwamba unasubiri kwanza-

-ripoti ya kiufundi ambayo ndio itatoa mwongozo, Mkongomani huyo ameishukia klabu hiyo na kumwaga kila kitu hadharani huku akieleza wamesajili wachezaji wa Ligi Kuu tu na si wa kimataifa.

Kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Pyramids ya Misri kwenye mechi ya mchujo ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba mwishoni mwa wiki, ndicho kilichowaibua mashabiki wa Yanga wakitaka Zahera atimuliwe.

Baadhi ya sababu ya mashabiki hao kutaka Zahera atimuliwe ni kutokana na timu kushindwa kuwa na muunganiko mzuri, kucheza ovyo pasipo maelewano, lakini wakieleza zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji wote waliosajiliwa ni kutokana na mapendekezo yake, hivyo kufanya vibaya kwa timu lazima abebe mzigo huo kwa kutimuliwa.  

Lakini juzi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, aliliambia Nipashe kuwa uongozi ulisikia "kilio" cha mashabiki wao, ila uamuzi wa kuachana na Zahera, bado haujazungumzwa na kwamba wanasubiri ripoti ya kiufundi ambayo ndio itatoa mwongozo wa hatima yake.

Akizungumza na gazeti hili jana, Zahera, alisema kikosi cha Yanga hakina mchezaji anayeweza kupambana katika mashindano ya kimataifa na wao walisajiliwa na kuandaliwa kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara tu.

Zahera alisema hakushangazwa na hajaumizwa na matokeo yaliyopatikana katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na "maneno" ya mashabiki hayamuumizi kichwa.

"Mimi ni kocha mwenye uzoefu mkubwa hapa barani Afrika, Yanga haina mchezaji hata mmoja mwenye hadhi ya kucheza Pyramids, hatukusajili wachezaji wa kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatukujiandaa na mashindano hayo, sisi tulisajili kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hatukuwa tayari kupambana," alisema Zahera.

Aliongeza kuwa mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuumia endapo watafungwa na klabu kutoka Burundi au Uganda na kamwe wasiumie pale wanapofungwa na timu kama Pyramids ambayo imejipanga na kujiandaa vema kupambana katika mashindano haya ya kimataifa.

"Mimi nilijiandaa kwa Ligi Kuu tu, nikiwa Afcon (Kombe la Mataifa Afrika), ndio nikaelezwa Yanga tunashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wachezaji tulionao ni wa kawaida, nasema hatukuwa tayari kushiriki mashindano hayo," alisisitiza kocha huyo Mmsaidizi wa zamani wa Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambaye mkataba wake na Yanga unatarajiwa kumalizia Septemba mwakani.

Aidha, Zahera alisema pia hana hofu ya kutimuliwa na vitendo vya kurushiwa chupa au kuzomewa na mashabiki ni vya kawaida kwenye maisha ya mpira wa miguu.

Wakati Zahera akieleza hivyo, mchambuzi wa soka nchini na Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Yanga aliyewahi kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio makubwa, Ally Mayay ameionya klabu hiyo akiitaka kuwa makini kwa maamuzi watakayoyafanya kuhusu kumtimua kocha huyo.

Mayay alisema ni kweli kwa sasa Yanga inacheza soka bovu ukilinganisha na msimu uliopita ikiwa na kocha huyo huyo ambaye kabla ya msimu kuanza alipewa nafasi ya kufanya usajili wa wachezaji anaowataka tofauti na aliowakuta msimu uliopita.

"Kwa zaidi ya asilimia 90 wachezaji waliopo Yanga ni kocha ndiye aliyependekeza wasajiliwe, hivyo mashabiki ni wazi walitegemea kuiona Yanga bora tofauti na ilivyo sasa, kinachoonekana ni timu kukosa muunganiko mzuri kwa sasa," Mayay alisema.

"Lakini suala la kumtimua Zahera kwa sasa linapaswa kufanywa kisayansi zaidi na kwa umakini wa hali ya juu kwani ni katikati ya msimu na ligi inaendelea hivyo kufanya mabadiliko kwa sasa, kunaweza kuharibu kila kitu."

Habari Kubwa