Kagere aishika Shy, Aussems afunguka

30Oct 2019
Somoe Ng'itu
SHINYANGA
Nipashe
Kagere aishika Shy, Aussems afunguka

KAGERE, Kagere, 'This is Simbaaaa, This is Simbaaaa! Ndio maneno yaliyokuwa yanatamkwa na wanachama na mashabiki wakati wanaipokea timu yao ya Simba ambayo wataishuhudia ikishuka kuwakabili-

-Mwadui FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini hapa.

Mshambuliaji wa kimataifa wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mnyarwanda Meddie Kagere na Miraji Athumani, wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongoza katika msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alisema wamekuja kushindana kama ambavyo walifanya katika mechi zilizopita za ligi hiyo inayoshirikisha timu 20 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Aussems alisema wanatarajia kukutana na changamoto kwa sababu kila timu inahitaji kupata matokeo mazuri na kujiweka kwenye nafasi nzuri na kutimiza malengo iliyojiwekea katika msimu huu.

"Tunatarajia kufanya mazoezi ya mwisho leo (jana) jioni, matumaini yetu ni kuwa na mchezo mzuri, lakini wenye changamoto na ushindani, hakuna mechi rahisi, timu zote zinajiandaa kusaka matokeo mazuri, na wachezaji wanajua ni nafasi yao ya kujitangaza na kuonyesha wanaweza," alisema Aussems.

Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Khalid Adam, alisema jana kuwa kikosi chake kiko imara na kimefanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo wa leo.

"Tunaijua Simba, tunajua wachezaji wake wanavyocheza, tumejiandaa kuwashangaza, tumepanga kuisimamisha, tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kutushangilia katika mechi hii ya kesho (leo)," Khalid aliliambia gazeti hili jana.

Habari Kubwa