Mshtakiwa kesi vigogo wa Nida ajisalimisha kwa DPP

30Oct 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Mshtakiwa kesi vigogo wa Nida ajisalimisha kwa DPP

XAVERY Silverius, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuomba kukiri kuhujumu na kuomba msamaha.

Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu

Silverius na wenzake wanne akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu, wanakabiliwa na mashtaka 55 likiwamo la kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 1.175.

Wakili wa Utetezi, Tully Kaundime, jana alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo ilipangwa kutajwa juzi, lakini upande wa utetezi ulidai una hoja ya kuwasilisha.

Kaundime alidai kuwa mteja wake aliandika barua hiyo Septemba 26, mwaka huu, lakini mpaka juzi walikuwa hawajapewa majibu kuhusiana na maombi hayo.

Kutokana na hali hiyo, wakili huyo aliomba upande wa mashtaka ueleze umefika hatua gani baada ya mteja wake kuwasilisha barua kwa DPP.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya, alidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, lakini Jamhuri inaomba kuwabadilishia washtakiwa hati ya mashtaka kwa kumwondoa mshtakiwa Astery Ndege.

Mahakama hiyo ilimhukumu Ndege kulipa fidia ya Sh. 293,446,400.23 baada ya kuandika barua ya kukiri makosa yake ya kutakatisha fedha.

Ndege ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, alilipa fidia hiyo ikiwa ni sehemu ya hasara iinayodaiwa kusababishwa na washtakiwa hao ya Sh. bilioni 1.175.

Hakimu Ally baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 11, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika hati mpya ya mashtaka ni Avelin Momburi, George Ntalima, Xavery Silverius, maarufu kama Silverius Kayombo, na Sabrina Raymond.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 55 yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu, kutakatisha fedha na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 1.175.

Habari Kubwa