Waziri Lugola ageuka trafiki kwa muda

30Oct 2019
Felix Mwagara
BUSEGA
Nipashe
Waziri Lugola ageuka trafiki kwa muda

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ameyakamata magari mawili yaliyotaka kusababisha ajali kwa kufukuzana na kulazimisha kuyapita-

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola (kulia), akimhoji dereva wa basi la abiria la Manoni Safari, Marijani Said (kushoto), ambaye alitaka kusababisha ajali kutokana na mwendo kasi huku akilazimisha kulipita gari lingine katika Kijiji cha Nyashishi, wilayani Busega, mkoa wa Simiyu jana.

-magari mengine bila ya kuwa na tahadhari katika Barabara Kuu ya Mwanza-Mara.

Magari hayo ni basi lililokuwa na abiria liitwalo Manoni Safaris lenye namba za usajili T800 DCU na lori namba T865 CVJ yaliyokuwa yanatokea Mwanza kuelekea mkoani Mara.

Akiwa safarini akitokea wilayani Bunda, waziri huyo alilazimika kuchukua hatua hiyo jana, magari hayo yalipofika katika Kijiji cha Nyashishi wilayani Busega mkoani Simiyu yakidaiwa kuwa kwenye mwendokasi.

Ilielezwa kuwa baada ya kushuhudia magari hayo yakiwa katika mwendokasi na yanalazimika kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, waziri huyo alimtaka dereva wake kugeuza gari na kuyafuatilia magari hayo.

“Huyu dereva wa basi hana tahadhari na ni mtu hatari sana, alitaka kutuua na pia kuua abiria wa basi hili, lazima afunguliwe mashtaka apelekwe mahakamani na iwe fundisho kwa madereva wazembe wa aina hii, na nimeambiwa na abiria hapa kuwa aliwapuuza baada ya kuambiwa apunguze mwendo,” alisema Lugola baada ya  kulisimamisha basi hilo.

Waziri huyo alimkamata dereva wa basi hilo, Marijani Saidi, na kumtaka atoe leseni yake na baadaye alipelekwa Kituo cha Polisi Busega ili kukamilisha taratibu za kufunguliwa mashtaka.

Waziri huyo pia aliagiza abiria wa basi hilo warudishiwe nauli zao na watafutiwe basi lingine ili waendelee na safari.

Akizungumzia tukio hilo, abiria wa basi hilo, Mwita Machela, alidai walimtaka dereva huyo kuacha kuendesha kwa mwendokasi, lakini aliwapuuza na kuendelea na safari.

"Waziri yuko sahihi kutusimamisha maana ametuokoa pia, huyu dereva alikua mwendokasi, tulimwonya aache, lakini hakutusikiliza, sasa haraka yake imeishia hapa, na sisi tumepotezewa muda wetu kutokana na uzembe wake,” alisema.

Waziri Lugola pia alimsimamia kondakta wa basi hilo akiwarudishia nauli abiria hao na kuhakikisha wanapandishwa katika mabasi yaliyokuwa yanapita katika barabara hiyo.

Habari Kubwa