James Mapalala, mwanasiasa ambaye hakukata tamaa kisiasa

30Oct 2019
Sabato Kasika
Nipashe
James Mapalala, mwanasiasa ambaye hakukata tamaa kisiasa

MWANASIASA mkongwe, James Kobelo Mapalala, ambaye alifariki dunia wiki iliyopita, ni miongoni mwa wanasiasa watakaokumbukwa kwa mchango wao mkubwa kwenye siasa za nchi hii.

Mzee James Mapalala (kulia), enzi za uhai wake akiteta jambo la Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Kimsingi historia ya harakati za demokrasia nchini haiwezi kukamilika bila ya kutaja jina la James Mapalala, kutokana na ukweli kwamba alikuwa miongoni mwa Watanzania wa mwanzo kabisa kudai mfumo wa vyama vingi nchini.

Historia inaonyesha kwamba akiwa katika harakati za kisiasa mwaka 1968, aliandika makala katika gazeti la Kiongozi, wakati huo akiwa anaishi Tabora akielezea kutoridhishwa na mateso wanayopata wananchi wakati huo.

Alikuwa akichukizwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa vijiji wakati huo kuwatesa wananchi na akaamua kuandika kilichotokea na kujikuta akikumbana na changamoto zilizosababisha kuswekwa ndani katika vituo mbalimbali vya polisi na hatimaye kuwekwa kuzuizini

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 1984 alimwandikia barua Mwalimu Julius Nyerere wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM akimtaka aruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini akajikuta matatani na kuwekwa kizuizini.

Mwaka 1986 alikamatwa tena na kupelekwa kizuizini mkoani Lindi, ambako alikaa hadi mwaka 1990, wakati huo akiwa amehamishiwa kisiwani Mafia mkoani Pwani.

Pamoja na matatizo hayo, hakukata tamaa kwa kuwa mawazo yake ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi yalikuwa palepale na alipotoka kizuizini, aliendeleza mawazo yake ya kuanzisha chama cha siasa.

Aliungana na wenzake na kuanzisha chama wakati ambapo hapakuwa na sheria ya vyama vingi, walienda kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, wakati huo Augustine Mrema na kumweleza nia yao hiyo.

Inasemekana Mrema alikuwa mkali na akawatimua, wakaamua kuandamana wakidai haki ya kuanzisha chama cha siasa wakiwa watu 35 na walipofika maeneo ya Kariakoo, watu waliongezeka hadi kufika 1,000.

Hata hivyo, polisi waliingilia kati na kuwakamata watu 25, huku yeye (Mapalala) akikimbilia Ubalozi wa Sweden kujificha, lakini waliokamatwa waligoma kula kwa siku kadhaa na kuanza kuitisha serikali.

Kitendo cha watu hao kugoma kilisababisha aingilie kati kuwabembeleza wale chakula tena kizuri kilichotolewa Kilimanjaro Hotel na kupelekwa gerezani.

KUANZISHA CHAMA SIASA

Wakati sakata hilo likiendelea, kulikuwa tayari kumeshajitokeza mabadiliko ya kisasa na kiuchumi ulimwenguni kufuatia mfumo wa ukomunisti kuanza kuanguka na ndipo baadaye alianzisha rasmi chama cha siasa.

Kwa ujumla, katika umri wake wa miaka 83, ambao Mungu alimjalia kuishi hapa duniani, historia inaonyesha kuwa mwanasiasa huyo alikaa kuzuizini miaka sita kwenye mikoa ya Kusini.

Hakukata tamaa, bali aliendelea na harakati zake za kisiasa bila kuchoka, kwani baada ya nchi kuridhia mfumo wa vyama vingi vya siasa, alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa vyama vya siasa.

Ninaweza kusema kuwa vuguvugu la vyama vingi lilirudisha kiu ya James Mapalala ya kuwatumikia wananchi, kwani mwaka 1991 alianzisha chama cha siasa kiitwacho Chama cha Wananchi  Tanzania (CCWT).

Wakati anaanzisha CCWT, kwa upande wa Zanzibar kulikuwa na Kamati ya Mabadiliko ya Kisiasa (KAMAHURU), iliyokuwa chini ya Shaban Mloo akishirikiana na Maalim Seif Sharif  Hamad.

Wanasiasa wengine wa kamati hiyo walikuwa ni Ali Haji Pandu, Hamad Rashid Mohamed, Dk. Maulid Makame na Soud Yusuph Mgeni, baadaye ikawa ni chama cha siasa kiitwacho Zanzibar United Front.

VYAMA VYAUNGANA

Mwaka 1992 baada ya kuruhusiwa kwa mfumo vya vyama vingi vya siasa, mkakati ulianza kwa kuangalia uwezekano wa kuunganisha Zanzibar United Front (ZUF) na Chama cha Wananchi (CCWT) cha Mapalala.

Historia inaonyesha Chama cha wananchi (CUF) kilianzishwa mwaka 1993 baada ya muungano wa vyama viwili; Zanzibar United Front (ZUF) kutoka Zanzibar na Chama Cha Wananchi Tanzania (CCWT) kutoka Bara.

Halmashauri kuu za vyama vyote zilikutana na kuanzisha nguvu ya pamoja mwaka huo, huku Mapalala akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa CUF na alianza rasmi kazi ya kukitangaza chama Bara na visiwani.

Mbali na Mapalala, viongozi wengine wa kwanza wa kitaifa wa CUF walikuwa, Makamu Mwenyekiti Maalim Seif Sharif Hamad wakati Katibu Mkuu akiwa ni Shabani Mloo.

Hata hivyo, badala ya muungano huo kuwa na nguvu, chama hicho kiliingia katika mgogoro, kukiwa na kundi lililompinga Mapalala, ambaye alimtuhumu katibu wake kwamba alikuwa akitaka kurejesha utawala wa kisultani Zanzibar.

Mgogoro huo ulimalizika baada ya Mkutano Mkuu wa CUF kufanyika mwaka 1994 na kumtimua Mapalala, nafasi yake ilishikiliwa na Musobi Mageni aliyechaguliwa mwaka 1995.

Mageni alishikilia nafasi hiyo ya mwenyekiti wa CUF taifa hadi mwaka 1999, ambapo mwanasiasa mwingine Profesa Ibrahim Lipumba akachaguliwa kushika nafasi hiyo anayoendelea nayo hadi sasa.

Kuondolewa kwa Mapalala kulitokana na viongozi wa CUF Zanzibar kuibua hoja kwamba ni msaliti, anafanya kazi mbili, ni mwenyekiti CUF lakini pia anatumika na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo kutofaa kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Mgogoro wa CUF ulifika kwa msajili wa vyama wakati huo, George Liundi, ambaye pia alikubaliana na tuhuma zilizoelekezwa kwa Mapalala, hivyo ukawa mwisho wa mwanasiasa huyo ndani ya chama hicho.

HAKUKATA TAMAA

Baada ya kutimuliwa ndani ya CUF, mwanasiasa huyo hakukata tamaa katika harakati zake za kisiasa, kwani mwaka 2001 alianzisha chama kingine kipya, Chama cha Haki na Ustawi (Chausta) akiwa ni mwanzilishi na mwenyekiti.

BUNGE MAALUMU

Mapalala aliendelea na harakati za kisiasa, na mwaka 2014 alikuwa miongoni mwa wanasiasa walioteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kupitia chama chake hicho cha siasa.

Moja ya kile alichokifanya katika Bunge bila kutoka kama walivyofanya wanasiasa wengine na kuanzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ni kukataa kupigia upatu serikali mbili, katika kamati yake namba moja.

Sababu kubwa aliyoeleza kuhusu msimamo wake huo ni kwamba serikali mbili zilikuwa zinamchefua, hivyo hakutaka kushiriki katika usaliti huo wa kuunga mkono serikali mbili na alipambana humo bungeni bila kutoka ndani.

Mbali na hilo, mwanasiasa huyo akawarushia dongo wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwamba walikuwa wakitengeneza mfumo wa kugawana posho kwa watu wa Tanzania Bara na Visiwani.

CHAUSTA YAFUTWA

Mwishoni mwa mwaka 2016, Chausta kilikuwa miongoni mwa vyama vitatu vya siasa vilivyofutiwa usajili, vingine vikiwa ni The African Progressive Party of Tanzania (APPT-Maendeleo) na Chama cha Jahazi Asilia.

Sababu za kufutwa kwa vyama hivyo zilielezwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuwa ni kutokana na zoezi la uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika Juni hadi Julai mwaka 2016.

Baada ya uhakiki huo ilibainika kuwa vilipoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa, na kila chama kilipewa nia ya msajili kufuta usajili wake, lakini vikashindwa kutoa utetezi wa kuridhisha ili visifutiwe usajili.

Kufuatia uamuzi huo, Msajili aliwataka waliokuwa wanachama wote wa vyama hivyo kutojihusisha na shughuli yoyote kwa majina ya vyama hivyo, na kwamba kufanya hivyo ingekuwa ni kuvunja sheria.

Tangu kufutwa kwa Chausta katika daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa, mwanasiasa huyo hakusikika tena katika harakati za kisiasa hadi taarifa za kifo chake zilipotangazwa.

Haijulikani kama Mapalala alijiunga na chama kingine cha siasa, na huenda akikaa pembeni ili kushuhudia jinsi harakati za kisiasa zinavyoendelea nchini baada ya yeye (Mapalala) kutoa mchango mkubwa kwa miaka mingi.

Hivyo kama nilieleza awali, katika siasa za nchi hii, Mapalala hawezi kuachwa pembeni, kwani ni miongoni mwa wanasiasa waliopoteza muda wao ili  Watanzania wawe huru kujiunga na chama chochote cha siasa wanachokitaka.