Mfumo wa Iran uliowekwa Iraq, Lebanon waanza kusambaratika

30Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mfumo wa Iran uliowekwa Iraq, Lebanon waanza kusambaratika
  • *Hata Washia sasa waisusa Hezbollah

KUNA viashiria kuwa nguvu ya Iran, inaanza kupungua katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya milipuko ya kisiasa na maandamano yasiyoisha kuzikumba Iraq na Lebanon, nchi mbili ambazo mfumo wake wa kisiasa unaitegemea Iran kwa kiasi kikubwa.

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Na Anil Kija

Nchi zote mbili zina makundi makubwa ya kijeshi yanayopokea amri kutoka Iran, huku mfumo wa utawala na mgawo wa rasilimali unategemea makundi ya kisiasa hasa yaliyo na majeshi yanaelekezwa kutoka Iran, na wanaweza kufikia muafaka wa utawala kwa kiwango gani na makundi mengine.

Kwa kawaida mfumo huo umekuwa ukifanya kazi lakini viashiria vya kuyumba kwake vinaongezeka.

Baadhi ya wachunguzi wa habari nchini Marekani wameanza kuunda hisia mpya kwa Iran, ina uwezo mkubwa wa kushawishi makundi yanayoendana na itikadi yake kutwaa madaraka nchi moja au nyingine, lakini siyo ufanisi katika kutumia madaraka hayo.

Siyo rahisi kusema kuwa tatizo liko katika uwezo wa kutawala au kutumia vyema madaraka ya nchi, kwani taasisi za serikali nchini Lebanon zimedumu kwa takriban miaka 30 tangu kumalizika kwa vita kati ya makundi tofauti ya kiitikadi nchini humo kuanzia mwaka 1975 hadi 1990.

Ni vita ambavyo watu 120,000 walipoteza maisha, zaidi ya milioni moja wakaondoka nchini kuhamia kwingine na hasa Ulaya ya Kusini na Magharibi, mpangilio mpya wa utawala ukakubaliwa, ukadumu hadi sasa.

Badala ya kudai kuwa Iran haina uwezo wa kushikilia hatamu za utawala baada ya kupata madaraka au makundi ya itikadi hiyo kushika hatamu za nchi, ni bora kuangalia jinsi Iraq na Lebanon zinavyokumbwa na wimbi la kutoridhika hasa miongoni mwa vijana.

Kama ilivyo barani Ulaya, Amerika ya Kusini katika nchi kadhaa, Mashariki ya Mbali huko Hong Kong na barani Afrika huko Sudan, Algeria na Misri (kwa sababu tofauti kiasi) hivi karibuni, ndiyo hali inayoinyemelea Iraq na Lebanon.

Suala muhimu la kimkakati ni kama Iran inamudu kutanzua hali hiyo, wakati nafasi yake ya kufanya biashara na kuingiza mapato imebanwa na Marekani.

Kilichowashangaza wafuatiliaji wa habari ni jinsi maandamano hayo yalivyoteka miji ya Lebanon kila upande wa nchi, na siyo tu jiji la Beirut, na cha msingi ni kuwa watu hawaridhiki tena katika nafasi ambayo kila jumuiya imepangiwa katika mfumo huo.

Wachunguzi nchini Marekani wanafikia tamati kuwa kinachosambaratika hivi sasa ni uwezo wa Iran kushawishi watu wa mataifa yanayoizunguka kuwa njia yake ya kiitikadi ndiyo bora na kutii mifumo ya utawala na mgawo wa majukumu kuelekea mikakati mipana ya kiitikadi.

Ndiyo inayotawala mwenendo wa Iran tangu mapinduzi ya mwaka 1979, yanayokwamishwa na kibano cha uchumi.

Iran ilishinda katika misukosuko mikubwa ya eneo hilo hasa kuanzia kuzuka kwa Uamsho wa nchi za Kiarabu mwaka 2011 na kuuawa Osama bin Laden mwezi Mei 2011.

Ilisaidia kuzuia kuondolewa utawala wa Syria licha ya kuwa nguvu kubwa zaidi ilikuwa ni ya Russia, na nchini Lebanon na Iraq vyama na makundi ya kijeshi tiifu kwa Iran yameendelea kushinda.

Tatizo kwa upande mmoja ni kuongezeka kwa vita, vikwazo na kupauka uchumi kutokana na mzingiro huo.

Wachambuzi katika jarida muhimu la Marekani kuhusu siasa za nchi za nje wanasema kuwa kwa miongo minne tangu mapinduzi ya 1979, watawala nchini Iran wamefaulu kutumia kila mwanya kupenyeza itikadi na kuunda makundi ya kisiasa yanayomiliki silaha, kulinda uwezo wao wa kutetea nafasi zao katika maeneo hayo.

Wanasema kuwa ambacho Iran haikuwahi kufikiria ni ‘visheni’ au mtazamo mpana wa kukua kwa uchumi na mahusiano ya kijamii katika hali hiyo, suala ambalo kwa anayeelewa mfumo wa fikra unaotawala Iran, halina msingi halisi.

Iran ni nchi inayoongozwa na itikadi ya ‘wilayat e fiqh,’ yaani utawala wa kuhani (mfikiriaji sheria ya dini aliye mahiri kati ya wenzake).

Ndiye anayesimamia serikali inayoundwa na shura, yaani Baraza la Wawakilishi linalochaguliwa na umati wa watu huku kanuni za msingi za mapinduzi zikifuatwa.

Kwa maana hiyo hapakuwa na haja ya kufikiria nini kitatokea katika uchumi na baada ya hapo Iran itafanya nini, kwani kila utawala uchumi duniani hutegemea kanuni za msingi za kuendesha nchi, kwa mfano demokrasia ya vyama vingi, au soko.

Kuwapo mabadiliko ya kina au ya ghafla ni kitu kinachotokana na historia kisichoweza kubuniwa mapema, lakini uwezo wa kukabiliana na hali kama hiyo unaendana na kile kilichokuwa kinatazamiwa awali.

Kwa upande huo ni wazi kuwa matazamio ya mapinduzi ya mwaka 1979 yalikuwa ni kuendelea kupata nguvu kwa itikadi ya kimapinduzi (ya dini, si yale ya kikomunisti) na kupungua nguvu kwa ‘ubeberu,’ mfumo wa nchi za Magharibi wa demokrasia, soko huria na kukamata rasilimali kote duniani.

Kimsingi, Iran ilikuwa na njozi ya itikadi ya mfumo wa jamii inayoutetea kukubalika kote Mashariki ya Kati.

Kimsingi hali hiyo ilifikiwa lakini haiwezi kudumu zaidi ya miaka 40, kwani kuna mkondo mkubwa zaidi wa uchumi ina maana kwa hiyo siasa ambayo unaeleweka katika fikra tofauti ya kimapinduzi, kuwa dunia nzima inataka maisha bora zaidi, yaani bidhaa bora kwa bei rahisi.

Ndiyo inakuwa utandawazi, kuwa nchi ikiwa na viwanda vyake vya teknolojia ya zamani na madeni lukuki ya kutafuta vipuri au spea za viwanda hivyo inajilundikia madeni, walanguzi wanapenyeza bidhaa bei poa, kodi zinazidi kwani nchi haina uwezo wa kununua vitu vingi kutoka nje.

Silaha kuu ya Iran ilikuwa ni mafuta, sasa teknolojia imebadilika hata Iran hivi majuzi ilipoipiga Saudia katika medani ya mafuta, bei yake haikupanda kubadili nauli kokote.

Ambacho pia kinaitesa Iran na watu wake au washiriki wa mfumo wake katika nchi kama Iraq na Lebanon kwa karibu na kwingineko kwa njia tofauti ni kuwa kupenya kwa teknolojia za habari na mawasiliano, zimerahisisha ushawishii wa kisiasa na kuunda mifungamano ya kutoa madai, na hata kubadili serikali.

Mtafaruku uliomwangusha hayati Rais Mohamed Morsi nchini Misri ilikuwa ni Bunge la Undugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood) wakiwa ndiyo wengi kupitisha marekebisho ya katiba kuwa umri wa kuolewa binti iwe ni miaka kuanzia 12, kwa ruhusa ya baba yake.

Nchini Sudan maandamano yalianza bei ya mikate ilipopanda wakati tayari watu wanapata tabu kumudu maisha, na nchini Lebanon serikali ilileta kodi mpya ya matumizi ya WhatsApp, mtandao unaopendwa kutumiwa na makundi ya kijamii ili kuzuia wasiwasiliane.

Kwa upande mwingine, unaweza kusema kuwa itikadi ya utawala nchini Iran kuanzia mwaka 1979 iliegeshwa katika dhana kuwa nje ya utawala huo kuna falme za Kiarabu ambazo pia zinashirikiana na Marekani kwa kina.

Mtazamo huo umekwamishwa na kuzuka kwa Dola ya Kiislamu na mkasa wa kuuawa yeyote asiyekubaliana na kila wanachosema – tatizo ambalo pia liliigusa Iran wakati wa mapinduzi kama ilivyo kwa mapinduzi kote duniani.

Sasa hatari ya kuzuka dola ya aina hiyo inaondoa ushawishi wa hisia kuwa unaweza kuunda ‘demokrasia ya kidini’ kwani huwezi kutabiri nani atachukua madaraka. Vijana wanataka ajira na uhuru, basi.