Vyama vilivyojipanga Kilimanjaro kushinda katika chaguzi zijazo

30Oct 2019
Mary Mosha
KILIMANJARO
Nipashe
Vyama vilivyojipanga Kilimanjaro kushinda katika chaguzi zijazo

NOVEMBER 24, mwaka huu, utafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.

Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, kunatarajiwa kuchaguliwa wenyeviti wa Mitaa 60, vijiji 519 na vitongoji 2,260, huku kukiwa na vituo vya uandikishaji 2,362.

Miongoni mwa vyama vya siasa vinavyotarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo mkoani Kilimanjaro ni pamoja na NCCR Mageuzi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Vyama vyote vya siasa vimeendelea kujigamba kuwa, kila kimoja kitashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi huo, na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwakani.

Pamoja na majigambo hayo, vyama  shiriki vya upinzani vinaonyesha wasiwasi kwa wagombea wao kutotangazwa endapo watashinda.

Vinatoa msimamo huo vikidai kuwa inatokana na matamko ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali na CCM, kuwa chama hicho kitashinda kwa namna yoyote.

NCCR

Katibu Mwenezi wa NCCR Mageuzi Taifa, Hemedi Msabaha, anasema wamejipanga kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mujibu wa katiba na kanuni.

Msabaha anasema, hiyo ni licha ya kuwa kinaamini kinakabiliwa na changamoto kubwa ya utaratibu na usimamizi kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa uandikishaji.

Anasema chama chao kimejipanga kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, na wanatarajia kushinda licha ya kuwa na changamoto za kimfumo, hasa kutokana na baadhi ya viongozi ambao hawamo kwa mujibu wa sheria.

Anabainisha kwamba, chama chao kinaona viongozi kama hao wanauingilia uchaguzi huo kwa kutoa matamko mbalimbali pamoja na kuwaaminisha wananchi kwamba wagombea wa CCM, watashinda kwa namna yoyote ile.

“Mwaka 2014, kulikuwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini katika jimbo la Vunjo tulifanikiwa kushinda vijiji 27 kati 78 na kwa sasa tunatarajia kushinda vijiji vyote na mitaa kwa asilimia 86 kwa Mkoa wa Kilimanjaro,” anasema na kuongeza:

“Kwani majimbo na wilaya zote tumesimamisha wagombea na kwa takwimu tutaziweka wazi…tunaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, tukiamini tuna changamoto nyingi hasa za vitisho.”

Msabaha anadai mfumo wa kiuchaguzi umeingiliwa na baadhi ya viongozi  ambao hawastahili kuingia kwenye uchaguzi na matamko ya baadhi ya viongozi wa chama tawala, yanaleta hofu ili wakate tamaa.

“Hata hivyo, hatutakata tamaa…kitendo hichi hakitafanyika kwa mara ya kwanza, kwani katika jimbo la Vunjo kwenye uchaguzi wa mwaka 2014, katika kijiji cha Duhuni, Kirua Vunjo Magharibi, alitangazwa mgombea  ambaye hakushinda kihalali,” anasema na kuongeza:

“Hali hiyo ilisababisha uvunjifu wa amani, miongoni mwa wananchi, kitendo ambacho si kizuri na kinakwamisha maendeleo.”

CCM

Kwa upande wake, Jonathani Mabia, Katibu wa CCM, Mkoa wa Kilimanjaro, anasema wamejipanga vyema kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Novemba 24.

Anasema chama hicho tayari kimemaliza mchakato wa kupata wagombea wa chama watakaoshiriki katika  kinyang’anyiro hicho, ngazi ya serikali za mitaa.

Anabainisha kutokana na utendaji uliotukuka wa serikali ya awamu ya tano, wanatarajia kushinda kwa asilimia 100.

“Sisi kama watendaji, tumehakikisha tumechagua viongozi wanaokubalika na wananchi katika kujituma na kuwaletea maendeleo… hatuna mashaka ya kushindwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa sababu kupitia Ilani ya CCM na utendaji wa serikali, umewaridhisha wananchi,” anasema. 

Mabia anabainisha kwamba kwenye chaguzi za mwaka 2014, ngazi ya serikali za mitaa, chama hicho kiliongoza kwa kupata idadi kubwa ya vijiji, vitongoji na mitaa.

“Tunatarajia kuendeleza historia hiyo kutokana na jitihada anazofanya mwenyekiti wa chama Taifa, Rais John Magufuli,”anasema.

Anabainisha kwamba wao wanashiriki kwenye uchaguzi huu kwa mujibu wa  sheria na kuionyesha dunia kuwa wanatekeleza demokrasia kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

TUHUMA ZA VYAMA

VYA UPINZANI

Akizungumzia tuhuma za vyama vya upinzani juu ya kutanganzwa kwa wagombea hata kama hawatashinda, Mabia anasema hilo halitegemewi.

“Vyama vyote vina uhuru wa kuweka mawakala wa kulinda hesabu na kusimamia kura za wagombea wao…lakini pia suala la kutangaza si la chama bali ni la kisheria,” anasema na kuongeza: 

"Chama kimefanya mambo makubwa kwa wananchi, hivyo hatutegemei kushindwa na badala yake tunatarajia ushindi wa asilimia 100.”

Mabia anatoa rai kwa vyama vya upinzani kutoogopa kuingia uwanjani, kwamba la muhimu kwa wote ni kufuata sheria na taratibu za uchaguzi, ili hatimaye apatikane mshindi atakayeweza kuwatumikia vyema wananchi.

“Tunasikia baadhi ya viongozi wanalalamika kuhusu muda uliowekwa wa kampeni, lakini CCM tunasema muda uliowekwa wa siku saba unatosha kwa sababu viongozi wanaochaguliwa wapo katika maeneo ya wananchi ambao wanajua nini wamewatendea,” anasema.

CHADEMA

Kwa upande wake, Chadema kinabainisha kwamba kutokana na jitihada walizofanya wanatarajia kupata ushindi kwa asilimia 80, katika mkoa wa Kilimanjaro.

“CCM imejitahidi kufanya siasa za chuki, lakini ukweli chama chetu kiko imara kwani kimejenga imani kubwa kwa wananchi katika kutetea maslahi yao,” anasema Katibu wa Mkoa, Basil Lema.

Lema anasema licha ya hali ya siasa nchini kuwa tete kitu kinacchosababisha baadhi ya wagombea katika baadhi ya maeneo kuogopa kusimama, lakini wameendelea na uhamasishaji na maeneo yote ya mkoa huo, wanagombea.

“Hakuna sehemu mgombea wa CCM atakayepita bila kupingwa kwani tumejipanga na tutashinda kwa kishindo kikubwa,"

WANACHAMA

Elisante Munuo ni mwanachama wa Chadema. Anasema mbali na changamoto ambazo wanakabiliana nazo yakiwamo matamko mbalimbali ya baadhi ya viongozi wa serikali na CCM, bado watafanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Changamoto ni nyingi lakini hatujakata tamaa, tutafanya maamuzi ambayo yataiacha CCM na baadhi ya viongozi wa serikali mdomo wazi,” anasema na kuongeza:

“Tumejipanga kushinda kwa asilimia 100, viongozi tulio nao wanajitahidi na tunawaamini.”

Naye Mariamu  Msuya, mwanachama wa CCM anasema kutokana  na jitihada za  mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dk. Magufuli za kuwatetea wanyonge na kupigania maendeleo, wagombea wengi  wa CCM watapita bila kupingwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, na uchaguzi mkuu mwakani.