Tuanze sasa udhibiti mbegu, pembejeo feki

30Oct 2019
Mhariri
Nipashe
Tuanze sasa udhibiti mbegu, pembejeo feki

MVUA zinazoendelea kunyesha licha ya kusababisha mafuriko kwenye maeneo mengine, ni fursa nyingine ya uhakika kwenye kilimo kwa sababu zimewahi na kunyesha kwa wakati.

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi mara nyingi mvua huchelewa, hunyesha kidogo na kwa miaka kadhaa mvua za vuli zimekuwa na changamoto nyingi kwani hazipatikani.

Mwaka huu kama ambavyo Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imekuwa ikitangaza, imeujulisha umma kuwa mvua ni nyingi na zitaendelea kunyesha kwa muda mrefu.

Tunaomba furaha ya mvua hii isiwe chanzo cha umaskini miongoni mwa wakulima ambao wanajikuta wakiuziwa mbegu feki.

Licha ya kwamba kuna wakala wa kudhibiti ubora wa mbegu TOSCI ni jukumu la mamlaka zinazohusika kuingilia kati na kuhakikisha kuwa wananchi hawadhulumiwa na kuuziwa mbegu zisizoota.

Ndiyo wakati ambao wakulima wanatarajia kuona kazi za wakala wa mbegu za kilimo (ASA) na TOSCI ukifanyakazi za kuwadhibiti wadanganyifu ambao mara nyingi husababisha hasara kwa wakulima. 

Ni ukweli kuwa wakulima vijijini na mijini mara nyingi wamejikuta katika tatizo la kuuziwa mbegu feki ndiyo maana nasi tunazikumbusha mamlaka za kuzalisha na kudhibiti mbegu kufuatilia ili kuepusha usambazaji mbegu duni kwa wakulima unaofanywa na wafanyabiashara wasio waadilifu.

Tunazikumbusha taasisi hizi wajibu wa kufuatilia kwa sababu mara nyingi mwanzo wa mvua kama hizi ambazo zimenyesha pengine bila wakulima kujiandaa ndiyo wakati wa wafanyabiashara wasio waadilifu kuwauzia mbegu feki wakulima ambao wengi walikuwa hawajajitayarisha kwa kilimo.

Lakini si mbegu tu na pembejeo nyingine kama mbolea na viuatilifu ambavyo kama vile mbegu zisizoota, hupewa mbolea ambayo hairutubishi mimea na kemikali ambazo hazitibu mazao wala kuua wadudu na visumbufu.

Pengine ASA na TOSCI haziwezi kufika kila mahali kwa wakati, lakini kuna vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) hivi viko kila kijiji na kila kata na hawa wanawafahamu wanachama wao, pia wanawajua wauza mbegu, mbolea na pembejeo.

Vyama hivi vina wajibu wa kusaka na kudhibiti wababaishaji hao na kufikisha taarifa ASA na TOSCI ili kuwakamata wahusika na kudhibiti mazoea hayo yanayosababisha hasara kwa wakulima wetu kila mwaka.

Tunahimiza ushiriki wa AMCOS kwa sababu baadhi ya wafanyabiashara wanatumia elimu ndogo na uelewa mdogo wa wakulima katika kutambua iwe mbegu, mbolea, au viuatilifu na kuwauzia bidhaa duni na feki.

Tunawakumbusha kuwa ni vyema kuweka kambi za kitaalamu na za wadhibiti kukagua mara kwa mara hasa kipindi hiki ili wanaouza pembejeo hizo wadhibitiwe mara moja na kuadhibiwa.

Tunashauri kazi kufanywa mapema ili kukabiliana na matokeo mabaya maana hakuna tija iwapo ukaguzi utafanyika na kuwabaini wahusika ambao tayari watakuwa wamewaumiza wananchi.

Ikumbukwe kuwa wakulima wanatumia gharama kubwa kuandaa mashamba, kununua mbegu, mbolea na viuatilifu na iwapo yote hayo yatakwamishwa na uuzaji wa pembejeo feki hakuna atakayesaidia kufidia wala kupunguza gharama hizo.

Pengine tunaona kwamba umefika wakati wa kukomesha mwenendo huu kwa kuwafungulia mashtaka ya kuhujumu uchumi watuhumiwa wa kuuza pembejeo feki ili kukomesha mazoea hayo yanayotishia hatima ya kilimo na ustawi wa wakulima wetu ambao wengi ni maskini.

Wakati mwingine kuna haja ya kuandaa sheria ya kuwabana wauzaji na wakulima kutumia mbegu za kisasa na watakaoshindwa kufanya hivyo kuadhibiwa ikiwa ni njia mojawapo ya kukomesha matumizi ya pembejeo na mbegu feki.

Tunaamini kuwa jitihada hizi zitasaidia kudhibiti kuuza mbegu na kupenyeza pembejeo feki zinazowaumia wakulima.

Habari Kubwa