Haya yakizingatiwa, uchaguzi serikali za mitaa ni mteremko

30Oct 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Haya yakizingatiwa, uchaguzi serikali za mitaa ni mteremko

KIPENGA kwa ajili ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa kilipulizwa jana, huku kukiwa na maelekezo ya kuzingatia kanuni za uchukuaji wa fomu hizo.

Uchukuaji na urejeshwaji wa fomu hizo unafanyika ndani ya siku saba na kufuatiwa na kampeni za uchaguzi zitakazodumu kwa muda wa siku saba na kisha uchaguzi kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Kampeni hizo zitatarajia kuanza Novemba 17 na kuhitimishwa Novemba 23 zikiwa zimefanyika kwa muda wa siku saba, ambao serikali inaamini unatosha kwa ajili ya uchaguzi huo.

Pamoja na kipenga kupulizwa, wadau wa uchaguzi, wakiwamo wagombea na vyama vyao, wamepewa maelekezo ya kuzingatia kwa lengo la kufanikisha mchakato huo.

Baadhi ya maelekezo hayo yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo,  ni lile linalowataka  wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha utoaji fomu hauingiliwi na changamoto ya aina yeyote.

Wasimamizi pia wanatakiwa kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake stahili ya kidemokrasia kama, ambavyo serikali inakusudia, ili kila mtu ashiriki katika uchaguzi huu bila kukwazwa na jambo lolote.

Kwamba ni muhimu  kusimamia kanuni katika mchakato mzima wa kuchukua na kurejesha fomu.

Katika mwendelezo wa maelekezo hayo, hairuhusiwi kufanya kampeni kabla ya siku iliyoanishwa na kwamba hata kama kuna mbwembwe wakati wa kuchukua fomu au kurejesha, zisiwe katika mtindo wa kampeni.

Vyama vya siasa navyo vinatakiwa kuhakikisha vinatumia vizuri demokrasia kwa kupeleka watu wanaowakusudia na kuwadhamini kwa mujibu wa kanuni, huku watendaji wa vijiji na mitaa wakiwa hawaruhusiwi kutekeleza jukumu lolote linalopaswa kuamuliwa kwanza na halmashauri za vijiji au mitaa.

Muungwana anaamini kwamba iwapo maelekezo hayo ya serikali yatazingatiwa na vyama vya siasa, hakutakuwa na malalamiko ambayo yamewahi kujitokeza kwenye chaguzi zilizotangulia.

Wagombea na vyama vyao, wasimamizi na wadau wengine wazingatie kile ambacho kimeelekezwa na serikali, ili Watanzania washiriki katika uchaguzi huo.

Hapa si kuchagua tu bali wawe huru kuchagua viongozi wanaowataka, na ndiyo maana wasimamizi wanatakiwa kusimamia demokrasia, ili kila mtu apate haki yake stahili ya kidemokrasia kama, ambavyo serikali inakusudia.

Hivyo kwa muda wa siku saba, ambazo zimewekwa kwa ajili ya mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu, ni muhimu wagombea na vyama vyao kuzitumia vizuri kwa ustawi wa demokrasia nchini.

Malekezo hayo yakizingatiwa yatakuwa yamezima malalamiko ambayo yamewahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuhusu wagombea kuwekeana mapingamizi kwa lengo la kukomoana.

Aidha, maelekezo hayo yanaweza kuondoa vilevile malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagombea kudai kuzuiwa kuchukua fomu au fomu zao kutopokelewa na wasimamizi.

Kwa maana hiyo Watanzania wanaotaka kushika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye serikali za mitaa, huu ndiyo wakati wao, lakini pia wazingatie maelekezo ya serikali.

Serikali inasema, katika uchaguzi huo hakutarajiwi kutokee changamoto ya aina yeyote, kwa vile jambo ambalo lilikuwa halijaeleweka vizuri, watu waliomba ufafanuzi na wakawa wamepewa.

Matarajio ya serikali ni kutaka wagombea wote wapatikane kwa haki kwa kuzingatia maelekezo ambayo imetoa kwa wadau wote wa uchaguzi.

Kuanzia wenyeviti wa vitongoji, katika mamlaka za miji midogo, mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi mchanganyiko la wanawake na wanaume) na wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi la wanawake) katika mamlaka za miji wanapatikana kwa haki.

Maelekezo hayo hayahusu wagombea hao tu bali hata wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa halmashauri za vijiji (kundi mchanganyiko la wanawake na wanaume), wajumbe wa halmashauri za vijiji (kundi la wanawake) na wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za wilaya.

Habari Kubwa