Sababu Mwadui kuitoboa Simba

01Nov 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Sababu Mwadui kuitoboa Simba
  • ***Dilunga atajwa kuwabeba wachimba madini hao, huku wakieleza mkakati alioundiwa Mzamiru kuhakikisha...

HUKU Simba ikiendelea kuugulia maumivu ya 'kutobolewa' (kufungwa) mechi yao ya kwanza kwenye Ligi Kuu msimu huu, Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Khalid Adam, amesema kitu kilichoifanya timu yake ipate pointi tatu katika mechi hiyo ni namna-

-walivyofanikiwa kuidhibiti idara ya kiungo ya mabingwa hao watetezi.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa CCM Kambarage juzi, Mwadui FC ilipata ushindi wa bao 1-0, kupitia kwa mshambuliaji wake, Gerald Mathias na kuondoka na pointi tatu zilizowafanya wafikishe idadi ya pointi 11 na kupanda hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha klabu 20 nchini.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Simba kupoteza, tangu msimu wa 2019/20 ulipoanza hapo Agosti 23, mwaka huu.

Akizungumza na Nipashe jana, Khalid, alisema ushindi wa mechi hiyo ulianza mapema baada ya kuona kikosi cha Simba kilichotangazwa kuanza katika mchezo huo kwa kutoliona jina la kiungo, Hassan Dilunga.

Khalidi alisema kuwa baada ya kuona "kikosi" hicho, aliwaambia wachezaji wake wanatakiwa kuhakikisha wanambana na kumdhibiti kiungo Mzamiru Yassin na watakapofanikiwa, watakuwa wamefaulu mchezo huo.

"Niliwaambia kwa kikosi hiki kilichopangwa, hapa anayepaswa kudhibitiwa ni Mzamiru, hii ndio "switch" ya Simba leo (juzi), kama mtafanikiwa kuizima, naamini ile furaha tuliyokuwa tunaitarajia, tutaipata, na walifanikiwa kufanya hivyo," alisema Khalidi, ambaye kutimuliwa na kurejeshwa katika kikosi hicho ni jambo la kawaida kwake.

Kocha huyo aliongeza kuwa, aliwaandaa wachezaji wake kutokuwa na woga, na kucheza kwa kujiamini na kwa kufanya hivyo, asilimia zisizopungua 70, walifanikiwa na kuwa klabu ya kwanza kuondoka na pointi msimu huu kutoka kwa mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo.

"Pia niliwaambia Simba ni timu kubwa, ina wachezaji wazoefu, lazima tuipe heshima yake, nashukuru makosa yalikuwa machache, sisi kwanza tulikuwa bora sana, ila nashukuru tumepata kile tulichokitarajia, halafu sikutaka kuwabana sana wachezaji, hata baada ya kumaliza mazoezi jana (juzi), tuliwaacha huru," Khalid aliongeza.

Naye beki tegemeo wa timu hiyo, Joram Mgeveke, alisema walikuwa makini na walikumbushana kufuata maelekezo ya kocha wao kila mara ili kuhakikisha wanapata ushindi.

"Siri ya ushindi ni kujituma kwetu, tulifuata maelekezo kwa kiasi kikubwa, hatukuwa na presha, tulijiandaa kupata matokeo mazuri, hata sare kwetu ilikuwa inatutosha, lakini tulisema ushindi pia unawezekana, tukaongeza juhudi na hatimaye tukafanikiwa," alisema Mgeveke.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wanashukuru Mungu wamemaliza mchezo salama na matokeo waliyopata yalitokana na kutocheza vizuri kama walivyokuwa wachezaji wa Mwadui FC.

"Mpira ndivyo ulivyo, tulitafuta nafasi tukashindwa kuzitimua, wenzetu wametafuta na kuitumia, unaweza ukashambulia na unaweza pia kushambuliwa, kuna mazuri tulifanya na makosa pia, mwalimu ameyaona, atayarekebisha kwa ajili ya mchezo unaofuata," alisema

Rweyemamu alisema kuwa, mchezo huo umemalizika, sasa wanarejea jijini Dar es Salaam ili kujiandaa kuwakaribisha Mbeya City kwa ajili ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Uhuru.

Habari Kubwa