Simba, Yanga zikiepuka haya, zitafanikiwa Caf

04Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Simba, Yanga zikiepuka haya, zitafanikiwa Caf

HATIMAYE mashabiki wa soka nchini wameshuhudia msimu mbaya kwa timu za Tanzania kuvurunda kwenye michuano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, Simba, Yanga na KMKM zote zimefanya vibaya kwenye Ligi ya Mabingwa wakati Azam, KMC na Malindi zikivurunda Kombe la Shirikisho Afrika. 

Hata hivyo, Yanga yenyewe ilijitahidi na kupenya raundi ya kwanza kabla ya kuangukia mechi ya mchujo kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilikutana na Pyramids FC ya Misri jana usiku. 

Licha ya kuangukia kwenye mechi hiyo ya mchujo hapakuwa na matumaini ya wawakilishi hao pekee wa Tanzania kimataifa kusonga mbele baada ya mechi ya awali, Yanga kukubali kipigo cha mabao 2-1 nyumbani katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. 

Na jana ilishuka dimbani nchini Misri kurudiana na Pyramids, lakini kukiwa na kukatishwa tamaa kwingi kutokana na Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera kuwa wa kwanza kukata tamaa.

Zahera aliwakatisha tamaa mashabiki, wanachama wa Yanga na Watanzania kwa ujumla baada ya kueleza hakuna mchezaji hata mmoja wa timu yake anayeweza kufananishwa kwa ubora na wale wa Pyramids. Lakini akaenda mbali zaidi kwa kueleza uwezo Yanga ni wakushindana na timu kutoka nchi kama Burundi na kwamba Pyramids ni ya kiwango cha juu sana kwao. 

Hakuishia hapo, kwani alifafanua zaidi kwamba wachezaji aliowasajili walikuwa ni kwa ajili michuano ya Ligi Kuu na si mechi za kimataifa kwa kuwa Yanga ilishtukizwa kushiriki michuano hiyo. 

Tayari mashabiki, wanachama na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wanataka Zahera atimuliwe kutokana na timu hiyo kuonyesha kiwango kibovu huku hadi sasa ikishindwa kuwa na muunganiko mzuri.

Lakini pia akitupiwa lawama kwa kauli yake hiyo wakati pia yeye akihusika katika usajili wa wachezaji kwa zaidi ya asili 90, jambo ambalo ni nadra sana kwa klabu mbili kongwe Simba na Yanga kuona kocha akihusishwa kwa kiwango kikubwa kama hicho katika usajili.

Ni kweli Zahera kama kocha amekosea kutoa kauli kama hizo wakati yeye akiwa kama 'Amiri Jeshi Mkuu' hakupaswa kuwa wa kwanza kukata tamaa wakati ana kazi kubwa ya kuliongoza jeshi lake vitani. 

Lakini sisi tunaamini pamoja na kubebeshwa lawama hizo, huu ni wakati wa klabu za Tanzania kujifunza kwa kuwa makini na aina ya makocha wanaowaajiri, lakini pia wachezaji wanaowasajili ikiwa ni pamoja na kuwa na timu ya muda mrefu.

Tunaamini mafanikio iliyoyapata Simba msimu uliopita kwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilichangiwa pia na kikosi chao kukaa kwa pamoja muda mrefu, lakini kitendo cha msimu huu kufanya mabadiliko makubwa ya wachezaji kukawagharimu hali inayoikumba Yanga kufuatia kikosi chao kuwa na nyota wengi wapya. 

Hivyo, hakuna haja ya kunyosheana vidole kwa sasa, bali klabu hizo zinapaswa kubadili sera zao za kubomoa kikosi kila msimu kwa kuwa na utamaduni wakuongeza wachezaji wasiozidi wanne ili kuwa rahisi kuzoena mapema kabla ya msimu kuanza.

Habari Kubwa