Hili la wachezaji wa Alliance Bodi ya Ligi isimung’unye kushusha rungu

04Nov 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Hili la wachezaji wa Alliance Bodi ya Ligi isimung’unye kushusha rungu

SIKUAMINI macho yangu kama nilikuwa naangalia moja kati ya Ligi Kuu kubwa kabisa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Ilikuwa kama naangalia mechi za mchangani maarufu kama ndondo ambazo nazo siku hizi mashabiki na wachezaji wake wameshaanza kustaharabika.

Ilikuwa ni jioni ya Alhamisi 31, Oktoba, kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kwenye mechi kati ya Alliance dhidi ya Mbeya City.

Mchezaji Israel Patrick alipata kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kufanya faulo ya ajabu kwa kumshika sehemu nyeti mchezaji mmoja wa Mbeya City.

Wakati mashabiki wote uwanjani na wale waliokuwa wakiangalia soka kwenye televisheni wakijadili tukio hilo, wengine wakitafakari, dakika ya 71, kipa wa Alliance John Mwenda naye akafanya kituko cha ajabu.

Alimkata mtama mchezaji mmoja wa Mbeya City akiwa hana mpira. Naye pia akaonyeshwa kadi nyekundu. Ilikuwa ni moja kati ya mechi iliyojaa utovu wa nidhamu wa hali ya juu kwa wachezaji wa Alliance.

Kwanza kabisa katika hili napenda kumpongeza mwamuzi wa mechi hiyo, Shomari Lawi ambaye aliwaonyesha kadi nyekundu za moja kwa moja wachezaji hao bila kupepesa macho. Labda kwa kuwa haikuwa mechi inayozihusu timu kubwa. Alifanya kazi yake vizuri.

Tukio hili likanikumbusha mechi kati ya Kagera Sugar dhidi ya Simba, mchezaji Zawadi Mauya alipomkata mtama mara tatu mchezaji wa Simba, Ibrahim Ajibu, ingawa yeye hakupewa kadi nyekundu.

Nikawa najiuliza kama baadhi ya wachezaji hapa nchini wanachukulia kuwa soka ni kazi au sehemu ya kwenda kutuliza matatizo yao kichwani. Kwa siku za karibuni kumekuwa na rafu za ajabu ambazo si za kimpira kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ninavyojua kuwa wakati mchezaji anacheza soka, pia awe analinda afya ya mchezaji mwingine kwa kutomchezea madhambi ambayo si ya kiungwana wala ya kimichezo yanayoweza kuhitimisha wasifu wake kisoka.

Lakini ninavyoona kuna baadhi ya wachezaji wa Kibongo hawajui hilo. Na kwa bahati mbaya hakuna hatua zozote za makusudi zinazofanya na Bodi ya Ligi ili kumaliza tatizo hilo.

Nilisema huko nyuma kuwa kitendo cha Bodi ya Ligi kutoa onyo tu kwa mchezaji Zawadi Mauya, basi kinaweza kufungua milango kwa wachezaji wengine kufanya uhuni kama wachezaji hao wa Alliance walivyofanya.

Kama Bodi ya Ligi ingetoa adhabu stahiki, sidhani kama kuna mtu angerudia na Zawadi angekuwa kama mfano kwa wachezaji wengine. Na kama Bodi ya Ligi ikiendelea na hili la wachezaji hawa kulifumbia macho na kutoa onyo, basi itegemee kuna baadhi ya wachezaji wataendelea na tabia hiyo wakiona hakuna chochote watakachofanywa. Mbele ya safari hatuombei, tunaweza kuona wachezaji wakichezeana rafu za kuvunjana miguu. Hivi mpaka tufike huko ndipo Bodi ya Ligi ikae na kutoa adhabu kali wakati tayari kuna mchezaji au wachezaji wameshavunjika au kuwa walemavu wa viungo na kukatisha ndoto zao kwenye soka?

Inabidi sasa Bodi ya Ligi iamke na kusawazisha mambo ili kuifanya Ligi ya Tanzania kuheshimika na kuvutia watu ndani na nje ya nchi, isionekana kama ni ligi ya mtaani kwa wachezaji kucheza kimtaani bila kufanya kitu.

Wachezaji wa aina hii ndiyo wanaosababisha kudharaulika kwa ligi kiasi cha kuwafanya baadhi ya wadhamini kukimbia kuwekeza kwenye soka kwa kuona kuwa soka ni mchezo wa kihuni.

Bodi ya Ligi iige kwa wenzao ambao hata siku moja hawakubali mchezaji yeyote kufanya uhuni au kucheza kihuni, badala yake wanataka wachezaji wenye vipaji na wenye kuonyesha uwezo wao uwanjani kwa ajili ya kuvutia wawekezaji na ndiyo maana ligi zao zinaheshimika na zina pesa.

Natarajia Bodi ya Ligi itafanya kitu kwa wachezaji hawa wa Alliance watovu wa nidhamu ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo na wanaotaka kuiga.

Habari Kubwa