Ushahidi wa Mbowe waibua mazito

05Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Ushahidi wa Mbowe waibua mazito

MWENYEKITI  Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amedai mahakamani kwamba upinzani umeshambuliwa katika matukio mbalimbali ikiwamo wanachama wake kuuawa, kujeruhiwa na kutekwa na mpaka leo hakuna taarifa wala watuhumiwa waliokamatwa na kushtakiwa mpaka sasa.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kushoto) na viongozi wenzake, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwamo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari 1 na 16, mwaka jana, jijini humo, walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika. PICHA: MIRAJI MSALA

Kadhalika, amedai chama chake kina lengo la kukibomoa chama tawala na kishike dola kuwaongoza Watanzania kwa kuwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanaongozwa na vyombo vya usalama likiwamo Jeshi la Polisi.

Mbowe alitoa madai hayo jana wakati akijitetea katika kesi ya uchochezi inayowakabili na wenzake wanane katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Akiongozwa na Wakili wa utetezi Peter Kibatala, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alidai kuwa pamoja na mambo mengine watu kadhaa akiwamo mwandishi wa habari Daudi Mwangosi aliyeuawa na askari polisi, jeshi hilo awali lilitoa taarifa kwa jamii kwamba ameuawa na Chadema.

Alidai kuwa baadhi ya viongozi wa chama chake akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Geita,  Alphonce Mawazo, aliuawa na mwili wake ulihifadhiwa katika hospitali ya Bugando, jijini Mwanza.

Alidai kuwa jeshi la Polisi lilizuia chama kufanye mazishi mpaka walipofungua kesi ya kuomba kibali cha kufanya mazishi hayo na kuruhusiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza lakini mpaka leo hakuna taarifa ya uchunguzi wa tukio hulo.

"Mheshimiwa hakimu msaidizi wangu, Ben Sanane, inasemekana alitekwa na vyombo vya dola miaka miwili na nusu iliyopita. Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alishambuliwa na watu wasiojulikana lakini mpaka leo hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo," alidai shahidi huyo wa kwanza wa utetezi.

Alidai kuwa chama chake kilijitahidi kuomba wachunguzi kutoka nje waje nchini kusaidia kuwabaini watu wasiojulikana lakini vyombo vya dola vilikataa.

Pia alidai kuwa jeshi hilo lilizuia mkusanyiko wa kufanya maombi kumwombea Lissu baada ya kupata majeraha makubwa na kwamba serikali na bunge havikushiriki kwa chochote katika kumsaidia matibabu mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki.

Akielezea uchaguzi mdogo wa  Jimbo la Kinondoni, alidai kuwa kiutaratibu mawakala wanatakiwa kupata nakala za utambulisho wa viapo siku saba kabla ya uchaguzi lakini kwa uchaguzi huo, kati ya mawakala 611  wa Chadema ni mawakala wasiozidi 60 ndio walipata nakala hizo.

Alidai kuwa miongoni mwa waliopata nakala hizo ni pamoja na Wakala Mkuu wa majumuisho, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Alidai kuwa kitendo cha mahakama kukosa utambulisho mpaka siku moja kabla ya uchaguzi, hakijawahi kutokea na kwamba alimlalamikia Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye alimjibu kwa maandishi kwamba haikuwa sahihi kukosa barua hizo.

kesi hiyo imepangwa kuendelea leo kusikilizwa ushahidi wa utetezi Mbowe.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo unaongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu Faraja Nchimbi, Joseph Kipande, Pendo Makondo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon, Mawakili wa Serikali Jacqueline Nyantori na Salum Msemo.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko;, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu; na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.

Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwamo la kula njama kwa madai kuwa Februari 1 na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walifanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.