RC ala nyama ya panya, ahamasisha ulaji wake

05Nov 2019
Hamisi Nasiri
MTWARA
Nipashe
RC ala nyama ya panya, ahamasisha ulaji wake

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, ameonyesha kwa vitendo udumishaji wa mila na desturi za baadhi ya wakazi wa mkoa huo kwa kula kitoweo cha panya hadharani. 

Aidha, Byakanwa aliwataka wakazi ambao wanakula kitoweo hicho sasa kula hadharani na hakuna sababu ya kula kwa kujificha kwani nyama ya panya inajenga afya.

Tukio hilo la Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kula panya alilifanya jana mkoani hapa akiwa na waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia kuhusu mila na desturi katika mkoa huo kwa lengo la kudumisha mila hizo.

Alisema ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera, na kwamba wakazi wa mkoa huo wana mila zao ikiwamo kula vyakula vya mila na utamaduni kama panzi aina ya senene, hivyo kila sehemu kuna aina ya vyakula vya asili.

Alisema ameamua kula panya ili kuhamasisha wale wote ambao wana utamaduni wa kula panya wasifikiri kama kitoweo hicho hakitambuli bali kinatambulika kama vyakula vingine vya asili.

Byakanwa alisema ingawa yeye mwenyeji wa Kagera, lakini kwa sasa ni kiongozi ambaye anawaongoza watu ambao baadhi yao mila na desturi  wanatumia panya kama chakula.

"Mimi leo nimekula panya na ukiniuliza kama ana radha gani nitakuambia kuwa ni mtamu sana, hivyo sasa nawaomba wale wote waliokuwa wanakula kwa kujificha wale hadharani," alisema Byakanwa. 

Alisema panya ni chakula kama ilivyo vyakula vingine na ndio maana wataalamu wa afya wanaeleza kuwa nyama ya panya ina virutubisho kama vilivyo kwenye nyama zingine za ng'ombe, mbuzi na kondoo.

Alisema kuanza sasa akiwa mkoani Mtwara ataendelea kula panya ili kuhamasisha mila na desturi za baadhi ya watu wa kusini wanaokula panya.