Yanga kimyakimya, Zahera sasa atetewa

05Nov 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Yanga kimyakimya, Zahera sasa atetewa
  • ***Mwakyembe aomba asitimuliwe kwani amepambana katika shida na raha, timu kujichimbia leo kwa...

WAKATI Yanga ikirejea jijini Dar es Salaam jana kimyakimya baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 nchini Misri dhidi ya Pyramids FC huku joto la mashabiki na wanachama bado likiendelea kufukuta wakitaka mkataba wa Kocha Mkuu Mwinyi Zahera sasa uhitimishwe-

Focus Nicus na Shufaa Lyimo

-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harisson Mwakyembe, ameitahadharisha klabu hiyo kuhusu kumtimua.

Matokeo hayo ya juzi, yanaifanya Yanga kuungana na watani na ndugu zao nchini, Simba, Azam, KMC, KMKM na Malindi kuiaga michuano ya kimataifa msimu huu baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 5-1 kwenye mechi hiyo ya mchujo ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hiyo ni baada ya mchezo wa awali uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Yanga kukubali kichapo cha mabao 2-1, ambapo vuguvugu la baadhi ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo lilianzia hapo wakitaka Zahera atimuliwe huku wakimrushia chupa za maji kwa kile walichodai timu kucheza bila kuelewana na kushindwa kuonyesha mchezo mzuri.

Juzi licha ya kusubiri kuiona mechi hiyo ambayo ilitarajiwa kuonyeshwa kupitia Azam TV kabla ya dakika 10 baada ya mechi kuanza kutangaza kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wao mchezo huo hautaonyeshwa, mashabiki sehemu mbalimbali na hata jana waliendelea kudai Zahera hastahili tena kukinoa kikosi hicho.

"Yaani tumepigwa ndani nje, na kutolewa kwa mabao mengi hivyo, lakini kubwa timu yetu ikishindwa kuelewana uwanjani hadi leo, kocha huyu wa nini sasa," alisema Juma Abubakar, mkazi wa Mbezi Luis jijini Dar es Salaam.

John Mathias wa Ubungo jijini Dar es Salaam, alidakia kwa kueleza: "Kuna haja ya kulibomoa benchi zima la ufundi kwani kocha kapewa nafasi ya kusajili wachezaji anaowataka na ameshindwa kupata matokeo huku timu ikicheza ovyo."

Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea mara tu ya kichapo cha kwanza na vuguvugu la Zahera kutaka kutimuliwa kuibuka, Waziri Mwakyembe aliliambia Nipashe kuwa Yanga haina budi kuachana na dhana hiyo kwa kuwa kocha huyo ni miongoni mwa makocha bora hapa nchini, ambaye ana kila sababu ya kupewa pongezi kwa kile anachokifanya.

Dk. Mwakyembe alisema hakuna sababu ya kutafuta mchawi wala kumtupia lawama kocha, bali wachezaji wanapaswa kujituma zaidi.

"Sioni sababu ya Watanzania kusema hawamtaki Zahera, ikumbukwe amepambana na Yanga katika kipindi cha shida na raha mpaka kuifikisha ilipo sasa," alisema Dk. Mwakyembe.

Katika hatua nyingine, baada ya Yanga kurejea jana mchana, wachezaji walipewa mapumziko kabla ya leo kuingia kambini kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Ndanda FC Ijumaa wiki hii.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, aliliambia Nipashe: "Timu imesharejea na inaingia kambini kesho [leo] kwa ajili ya safari ya Mtwara."

Habari Kubwa