Hongera awamu ya 5 imefanya yaliyotukuka

05Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Hongera awamu ya 5 imefanya yaliyotukuka

SERIKALI ya Rais John Magufuli, inapomaliza kipindi cha miaka minne, Tanzania inashuhudia mambo makubwa yaliyoleta mafanikio kwenye sekta zote kuanzia uchumi hadi ulinzi na usalama.

Ujenzi wa miundombinu kama reli ya kisasa, viwanda, ununuzi wa ndege zinazofanya safari za ndani na za kimataifa, kuboresha sekta ya  jamii ikiwamo elimu ni mambo yanayoiweka Tanzania kwenye orodha ya mataifa  yanayobadilika kwa kasi.

Tunawapongeza Rais Magufuli, Makamu wake, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa. Tunaona kuwa kila Mtanzania anapoulizwa swali kuhusu  utendaji wa awamu ya tano anajibu moja kwa moja kwa kutaja kazi zinazofanywa na  viongozi hawa.

Tunapenda kuipongeza serikali kwa mafanikio mengi kuanzia kutatua changamoto za ardhi na kumaliza migogoro mingi iliyokuwa inatatiza sekta hii na kusababisha usumbufu mwingi mikoani, vijijini hata miongoni mwa wawekezaji.

Awamu ya tano imekuwa kielelezo cha mafanikio kwenye  uwajibikaji uliotukuka na kuhakikisha kuwa viongozi wanafanyakazi kwa mujibu wa kanuni na sheria za utumishi wa umma.

Aidha, kwa namna ya kipekee tunapenda kugusia hatua za hivi karibuni za kuzishughulikia moja kwa moja changamoto kubwa zinazowatatiza wananchi wa vijijini na mijini kwenye maeneo ya  miundombinu pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji.

Tunapoungana na Watanzania kuadhimisha miaka minne ya Awamu ya Tano, tunaipongeza hatua ya kipekee ya kuanzisha Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) ambaye amepewa jukumu muhimu la kujenga na kukarabati barabara za mijini na vijijini ambazo siku za nyuma zilikuwa zinashughulikiwa na halmashauri.

Uwapo wa Tarura ni mafanikio makubwa kutokana na ukweli kuwa ujenzi wa barabara, madaraja na makalavati ambayo pengine kutokana na urasimu kazi hazikufanikiwa kama ambavyo Tarura sasa imesimama kidete.

Tunaipongeza awamu hii kwa kuhakikisha kuwa pamoja na barabara kuu na za kitaifa kuiunganisha mikoa na nchi jirani, wilaya zote,  vijiji na mitaa mijini na vijini hazijasahaulika zinaunganishwa na kuimarishwa jukumu linalofanywa na Tarura.

Watanzania wana kila sababu ya kufarahia na kusherehekea mazingira na maeneo wanayoishi kwa sababu barabara zimeboreshwa na kuziwezesha  jamii kusonga mbele kwa kurahisishiwa usafirishaji uwe wa watu, mazao na pembejeo na hilo sasa si tatizo tena.

Kila mmoja  anayependa maendeleo na anayefahamu kuwa Tanzania ya sasa si ya kutegemea uhisani bali ni ya kutumia rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo ya raia wake.

Ndiyo maana tunazidi kuipongeza serikali kuwa na jicho la tatu kwenye sekta ya maji. Kuundwa Mamlaka ya Maji Vijijini ambayo haiingiliana na Mamlaka za Maji Mijini kama DAWASA kwa Jiji la Dar es Salaam ni hatua kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Kwa miaka minne tumeshuhudia umakini wa serikali katika mapambano dhidi ya rushwa. Bila kupiga vita rushwa, nchi haiwezi kupata maendeleo kwa kuwa rushwa ni adui mpya wa Taifa baada ya maadui watatu waliotajwa baada ya Uhuru ambao ni maradhi, ujinga na umaskini.

Safu hii haitoshi kueleza mafanikio yote ya miaka minne, lakini tumalizie kwa kupongeza utoaji wa elimu bure kwa elimu ya msingi na sekondari, hivyo kuwezesha watoto wengi wa maskini wakipata fursa ya kusoma.

Hongera awamu ya tano kwa kuongeza uwajibikaji na utumishi uliotukuka kwa kuhakikisha wenye dhamana wanatimiza wajibu na kuwatumikia Watanzania

Hongera Rais Magufuli, Samia na Majaliwa. Mungu azidi kuwabariki na kuineemesha Tanzania.

Habari Kubwa