Kidato cha nne, imalizeni safari yenu kwa mafanikio

05Nov 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Kidato cha nne, imalizeni safari yenu kwa mafanikio

JUMLA ya watahiniwa 485,866 wakiwamo wavulana 229,838 na wasichana 256,028 wameanza mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, ikiwa ni mwisho wao wa kupata elimu bure kulipa ada.

Hii inatokana na utaratibu uliowekwa na serikali wa kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne na sasa hatua inayofuata ni wazazi kulipa ada mara watoto wao watakapofaulu kuendelea na masomo.

Ni jambo jema kwa wanafunzi kuzingatia kile ambacho wamejifunza wakiwa shuleni na kukifanyia kazi.

Ninasema hivyo, kwa sababu kumekuwa na taarifa kwa nyakati tofauti ya baadhi yao kuchora vitu vya ajabu, kufutafuta au kuchora picha wanazojua wenyewe kwenye karatasi za mitihani.

Ndipo hapo Muungwana anaposhangaa kuona mwanafunzi wa sekondari akiamua kufanya uhuni wa aina hiyo, hali inayoonyesha kwamba hajui umuhimu wa elimu.

Wanafunzi wanaohitimu sasa ni wale ambao wamefaidika na utaratibu wa serikali wa kutoa elimu bure, ulioanza mwaka 2016 wakati wao wakiwa kidato cha kwanza, hivyo fursa hiyo isiishie kidato cha nne.

Serikali imeshaweka wazi kwamba inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu na kwa sababu hiyo na ndio maana mwaka 2019/20 imetenga bajeti ya Sh. bilioni 288.485 kutekeleza mpango wa elimu bila malipo.

Ikumbukwe kuwa tangu mpango huo wa elimu bure uanze mwaka 2016, serikali imeshatumia Sh. bilioni 937.54 kugharamia elimu ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.

Juhudi hizo ni za kuunga mkono na wanafunzi kwa kufanya vizuri katika mitihani badala ya kufanya madudu kama ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Kutokana na umuhimu wake, elimu imekuwa na kaulimbiu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulinganishwa na ufunguo na nyingine nyingi kwa kutambua kwamba mafanikio kwa kila mtu mara nyingi huletwa na elimu.

Ndiyo maana wazazi na walezi wote wanapaswa kuwahimiza vijana wao wasome kwa kutambua kuwa wao ni taifa la kesho ama nguvu kazi ya taifa hili kwa baadaye.

Jambo la muhimu ni wadau wote wa elimu wakiwamo wazazi na walezi kuhakikisha wanawahimiza watoto wote walioandikishwa kufanya mtihani huo wanafanya bila kukosa.

Kwani wanafunzi wa kidato cha nne wanapofanya mtihani wanatakiwa wajitambue wao ni nani na wanatarajia nini baadaye kuliko kufanya madudu ya kukusudia.

Vilevile watambue kuwa elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo binafsi pia taifa kwa ujumla, hivyo waamue kwamba miaka yao minne waliyokaa shuleni haipotei bure na badala yale waitendee haki kwa kufanya mitihani ya taifa kikamilifu.

Wafanye wakitambua kuwa viongozi wa taifa la kesho wanatokana na wao, na bila kuzingatia hilo wanaweza kujikuta kwamba miaka yao minne shuleni haikuwa na tija.

Kama anavyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kuwa viongozi na watendaji wote washiriki kwenye usimamizi na uendeshaji wa mitihani hiyo, basi watimize wajibu.

Waziri anawataka wafanye kazi zao kwa weledi, maadili na kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za usimamizi na uendeshaji wa mitihani hiyo kama ilivyoelekezwa na Necta.

Kwa utaratibu huo anaoelekeza waziri, ni wazi kwamba tatizo la kuwapo kwa baadhi ya wanafunzi wanaofanya vituko vya makusudi kwenye mitihani wanaweza kupungua kama siyo kumalizika kabisa.

Ingawa kuna urithi wa vitu mbalimbali ambavyo mtoto anaweza kupata kutoka kwa wazazi wake, urithi mkubwa na wa maana ni elimu na ndiyo imekuwa ikisisitizwa na wadau wa elimu.

Hivyo ni wajibu pia kwa kila mwanafunzi kuitendea haki elimu anayopata, tangu anapoanza shule hadi kwenye mitihani ili iweze kuwa na manufaa kwa maisha yake ya baadaye anapoingia uraiani.

Habari Kubwa