Zahera amwaga upupu akitimuliwa

06Nov 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Zahera amwaga upupu akitimuliwa
  • ***Asema anaidai Yanga mamilioni na hakuwahi kupewa malengo katika klabu hiyo, Mkwasa apewa timu huku...

BAADA ya uongozi wa Yanga kutangaza kuachana na Kocha wao Mkuu, Mwinyi Zahera, Mkongomani huyo amemwaga 'upupu' akieleza hafahamu chochote kuhusu kutimuliwa kwake na kwamba kwanza klabu hiyo ilipaswa-

Shufaa Lyimo na Jumanne Juma

-kwanza kumlipa mamilioni yake anayoidai na kufuata utaratibu uliopo katika mkataba wake vinginevyo atawashtaki.

Uongozi wa Klabu ya Yanga kupitia kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla akiambatana na Makamu Mwenyekiti wake, Fredrick Mwakalebela, jana ulitangaza kuachana rasmi na Zahera pamoja na kuvunja benchi zima la ufundi na nafasi ya kocha huyo mkuu sasa itachukuliwa kwa muda na Boniface Mkwasa.

Lakini Nipashe lilipomtafuta Zahera, baada ya Yanga kutoa taarifa hiyo, alisema kama angekuwa ana taarifa ya kuvunjiwa mkataba wake asingefanya mazoezi ya asubuhi na timu hiyo aliyokuwa akiiandaa kuelekea mechi yao dhidi ya Ndanda FC.

“Mimi sijapata barua yoyote kutoka Yanga kuwa wameachana na mimi kwa sababu nilikuwa kwenye mazoezi ya asubuhi na wachezaji wangu nikijiandaa na mchezo wetu wa Ligi Kuu dhidi ya Ndanda FC ambao tulikuwa tucheze Novemba 8, mwaka huu,” Zahera alisema.

“Binafsi sijaona sababu ya Yanga kunivunjia mkataba wangu kwani hawajakaa na kuzungumza na mimi chochote wakati bado nina madeni yangu mengi ambayo hawajanilipa na niliyowalipia wachezaji, iweje watangaze kuvunja mkataba bila kufuata taratibu mtu akikuvunjia mkataba lazima utaratibu wa mkataba ufuatwe.

"Ninataka nipewe barua iliyoambatanishwa na sababu zilizowafanya wao kwa nini waamue kuvunja mkataba na baada ya hapo nitazungumza kwa kina na vyombo vya habari, ili wadau na mashabiki wa timu hii wajue kile kilichokuwa kinaendelea baina yetu na uongozi."

Alisema hata walipokuwa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika nchini Misri, Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Dk. Msolla alimwahidi kutokumfukuza hata kama wakitolewa kwenye michuano hiyo.

Zahera alisema wakati anasaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo hajapewa malengo yoyote ya kuhakikisha timu hiyo inapata ubingwa kwenye mashindano ya kimataifa na kudai siku zote alizokaa na klabuni hapo hajaona dalili kama angekuja kufanyiwa hivyo.

“Tangu nirudi au leo asubuhi sijaona wala kusikia fununu yoyote ile kuwa ninafukuzwa ndani ya Yanga ndio maana naomba mvute subira mpaka nitakapopata barua nitasema yote kwa sababu nikisema mengi sasa hivi watanigeuzia maneno,” alisema.

Awali akitangaza uamuzi wa kuachana na Zahera na kuvunja benchi zima la ufundi, Dk. Msolla alisema wameamua kuachana na Zahera baada ya kuona timu inakwenda vibaya.

"Tumeamua kuachana na Zahera baada ya Kamati yetu ya Utendaji kukutana kwa pamoja na kukubaliana na maamuzi hayo," alisema Msolla na kufafanua. "Tumeachana na Zahera kwa amani kabisa bila chuki yoyote lengo ni kupata kocha mzuri mwenye vigezo."

Aliongeza kuwa mkataba wa Zahera ulikuwa umalizike Septemba mwakani na wa Kocha Msaidizi, Noel Mwandila unatarajiwa kumalizika Desemba 3, mwaka huu.

Yanga ambayo imetolewa na Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 5-1 kwenye mechi ya mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, inashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi saba baada ya kushuka dimbani mara nne ikishinda michezo miwili, sare moja na kupoteza mmoja.

Habari Kubwa