Simba, Prisons hakuna mbabe

08Nov 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Prisons hakuna mbabe
  • ***Maafande hao waendelea kushikilia rekodi ya kutopoteza mchezo msimu huu...

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba wamelamizimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya "Maafande" wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya, katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Beki wa Simba, Shomari Kapombe (kulia), akimiliki mpira huku akizongwa na wachezaji wa Tanzania Prisons katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana. Mechi hiyo iliisha kwa suluhu. PICHA: JUMANNE JUMA

Ulikuwa ni mchezo uliotimua akili na nguvu hasa kwa Prisons ambao walikuwa wakitumia njia zote kuhakikisha haifungwi, na inamaliza kwa kushinda mechi au kutoka sare, jambo ambalo walifanikiwa.

Matokeo ya mechi hiyo yameifanya Simba, kupata sare yake ya kwanza kwenye katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ikicheza mechi tisa, kushinda saba, kupoteza moja na sare moja wakati Prisons imeendeleza rekodi yake safi ya kutopoteza mechi yoyote mpaka sasa, ikiwa imecheza mechi 11, ikishinda mechi nne na sare saba.

Simba bado inaendelea kuongoza ikiwa na pointi 22, huku Prisons inayofundishwa Adolph Rishard na ikishika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 19.

Kipindi cha kwanza Prisons iliishinda Simba kwa kufanya mashambulizi ya hatari zaidi kwenye lango la mabingwa hao watetezi.

Ilianza kulitia msukosuko lango la Simba dakika ya 11 tu wakati Salum Kimenya alipopata krosi safi akiwa hajakabwa na beki yoyote wa timu pinzani, akaachia shuti lililotoka pembeni kidogo mwa lango la wapinzani wao.

Dakika ya 31, lango la Simba lilikuwa kwenye majaribu wakati straika wa Prisons, Jeremiah Juma, aliingia ndani ya eneo la hatari, lakini alichelewa kupiga mpira na kukutana na kipa, Aishi Manula ambaye katika harakati za kuudaka ulimponyoka na kuambaambaa kama unaeelekea wavuni, lakini ghafla mpira ulibadili uelekeo na kwenda pembeni mwa lango, kabla ya mabeki kuuokoa na kuwa kona tasa.

Jaribio pekee la hatari la Simba lilifanywa dakika ya 39, wakati Meddie Kagere alipoaambaa na mpira winga ya kushoto na kupiga krosi iliyokatika na kutaka kujaa wavuni, lakini ukaokolewa kwa ustadi na kipa, Jeremiah Kisubi.

Kipindi cha pili karibuni chote, Prisons waliamua 'kupaki basi', na kushambulia kwa kushtukiza kitu kilichoifanya Simba kushambulia mfululizo, lakini wachezaji wake walishindwa kuipenya ngome ya wapinzani wao ikiongozwa na Nurdin Chona.

Ilifanya majaribio dakika ya 56, Deo Kanda, alipopiga mpira juu akitazamana na kipa, Kagere naye aliukosa mpira wa krosi ambao ungeweza kuipa timu yake goli, huku kinda, Rashid Juma, alipoikosesha timu yake bao, baada ya kupiga shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari lililotoka kidogo pembeni mwa lango.

Dakika ya 72 nusura Prisons iandike bao, baada ya Samson Mbangula kubaki wa kipa Manula, lakini kipa huyo aliokoa kwa ustadi na dakika ya 87 pia walikosa bao la wazi kupitia kwa Lambart Subianka.

Ligi hiyo ya juu nchini inatarajia kuendelea tena leo kwa Ndanda FC kuwakaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara wakati Azam FC itawaalika Bishara United kutoka Musoma huku Kagera Sugar wakiwa wageni wa KMC FC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam.

Habari Kubwa