Ni aibu kuruhusu uhalifu huu wa kilimo cha bangi

08Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Ni aibu kuruhusu uhalifu huu wa kilimo cha bangi

WAKATI zikitolewa taarifa za kupungua kwa matukio ya utumiaji, usafirishaji na uuzaji wa dawa mbalimbali za kulevya nchini, bado kuna changamoto kutokana na kasi kubwa ya ulimaji wa zao la bangi.

Taarifa za sasa zinaonyesha kuwa baadhi ya mikoa inaongoza kilimo hicho, hivyo kuashiria kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayanabudi kujielekeza katika kudhibiti kilimo cha bangi ambacho kinachochea biashara na matumizi yake katika jamii yetu.

Serikali imesema kwamba matumizi ya dawa za kulevya aina ya bangi, bado ni tatizo nchini, huku mkoa wa Mara ukitajwa kuwa ni kinara katika kulima zao hilo ukifuatiwa na Tanga.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ndiye aliyebainisha hayo bungeni juzi, wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya dawa za kulevya kwa mwaka 2018.

Mhagama alisema pamoja na jitihada zilizofanywa na serikali katika kupambana na dawa za kulevya nchini, bangi imeendelea kuwa tatizo kubwa nchini na kuitaja mikoa mingine inayolima kwa wingi zao hilo ni Morogoro, Arusha, Kagera na Ruvuma.

Katika kuonyesha ukubwa wa jambo hilo, Mhagama alisema kwamba kwa kipindi cha mwaka 2018 juhudi za vyombo vya dola kwa kushirikiana na wananchi zilifanikisha ukamataji wa tani 24.3 za bangizikiwahusisha watuhumiwa 10,061.

Alisema dawa za kulevya aina ya mirungi nayo imeendelea kutumiwa na watu wa rika mbalimbali, kwamba kwa mwaka 2018 vyombo vya dola vilikamata tani 8.97 za mirungi zikiwahusisha watuhumiwa 1,186.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2018, kesi 7,592 zikiwa na watuhumiwa 10,979, zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali, kesi 7,174 zilizowahusisha watuhumiwa 11,045 ziliendelea kusikilizwa.

Sisi tunafikiri kuwa kilimo cha bangi kinaweza kukomeshwa kabisa ikiwa jamii nzima itaamua kushirikiana badala ya kuliachia Jeshi la Polisi pekee jukumu hilo.

Tunasema hivyo kwa kuwa wahusika ni wananchi wenyewe na bangi hiyo inalimwa katika mashamba ambayo yako kwenye maeneo yao, hivyo wanazo taarifa zote kuhusiana na wamiliki wa mashamba hayo pamoja na wanaoilima pamoja na kufahamu wanaivuna wakati gani na wanaipeleka wapi kuiuza.

Wananchi hawapaswi kujivua lawama hizo kwa kuwa huko nyuma tumekuwa tukishuhudia Jeshi la Polisi likienda katika maeneo mbalimbali kufyeka mashamba ya bangi na kuiharibu baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Mbali na ushirikiano wa jamii nzima na vyombo vya dola wa kupeana taarifa kuhusu wanaojihusisha na kilimo cha bangi, njia nyingine ni ya kukaza sheria kuhusiana na bangi.

Hapa tunamaanisha kuwa serikali inaweza kutunga sheria kali ya kudhibiti kilimo hicho kwa kuwabana kwa adhabu kali wamiliki wa mashamba ambayo yatalimwa bangi.

Pia viongozi wa serikali ngazi za vijiji, vitongoji na mitaa wapewe jukumu la ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mashamba yanayotiliwa shaka kutumika kwa kilimo cha bangi.

Tukibaki kulalamika kuwa uzalishaji wa bangi unaongezeka na kutaja tu mikoa inayoongoza, tutakuwa hatulisaidii taifa, bali tutakuwa tunaviacha hatarini vizazi vijavyo kwa kuwa athari za bangi na dawa nyingine za kulevya tunazifahamu.

Habari Kubwa