Mungu ibariki Stars kuelekea Afcon 2021

11Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Mungu ibariki Stars kuelekea Afcon 2021

KWA mara nyingine tena, Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), inatarajia kushuka dimbani Ijumaa kuwakabili wapinzani wao kutoka Equatorial Guinea.

Stars itawakaribisha wageni hao Ijumaa, kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam, ikiwa ni mechi ya kwanza ya kuanza safari ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2021).

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mrundi Etienne Ndayiragije anayeshirikiana na Juma Mgunda kutoka Coastal Union na Selemani Matola wa Polisi Tanzania, kinaanza kampeni hiyo mpya kikiwa tayari kimepata tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Stars inaingia kuanza kampeni hiyo pia ikiwa na kumbukumbu ya kucheza fainali zilizopita na Afcon, zilizofanyika Juni mwaka huu nchini Misri, ikiwa ni baada ya kuikosa michuano hiyo kwa miaka 39.

Katika kuhakikisha kuwa Stars inaendelea kufanya vema katika mashindano mbalimbali inayoshiriki, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limejaribu kuipa maandalizi ya kiwango cha juu, yanayofanana na hadhi ya timu hiyo ambayo inapeperusha bendera ya nchi.

Tunawakumbusha kuwa, kilichotokea hadi Stars itapata tiketi ya kushiriki fainali zilizopita na kufuzu CHAN kwa mara ya pili, kinatakiwa kifanyike mara mbili au tatu, ili timu hiyo iweze kupata matokeo mazuri katika mechi zake.

Wachezaji wote walioitwa katika kikosi hicho, wanatakiwa kuweka uzalendo mbele, kwa kujituma na kupambana ili wapate matokeo chanya ambayo yataipeleka timu hiyo Cameroon na kuwa moja ya timu zitakazowania ubingwa wa Afrika.

Hakuna kisichowezekana, nguvu na juhudi zilizowapeleka Afcon Misri, zinatakiwa ziongezeke ili isionekane Tanzania ilibahatisha kushiriki mashindano hayo ya juu hapa barani Afrika.

Wachezaji wasifikiri kutangaza jina la Tanzania, wanatakiwa wafikirie mashindano hayo, ni daraja lao la kuelekea kwenye mafanikio, kwa sababu mawakala kutoka nchi mbalimbali hufika kutazama vipaji, na kwa maana hiyo, nyota watakaofanya vema watakuwa wamejitengenea soko.

Kila mchezaji ana ndoto zake, na ndoto kubwa ni kwenda kucheza Ulaya au kupata klabu ya kuitumikia iliyoko nje ya Tanzania ambayo tunaamini, itamlipa mchezaji huyo mshahara na posho bora zaidi ya kile alichokuwa analipwa hapa nyumbani.

Lakini njia za kufika huko ni tofauti, wengine wanapata fursa kupitia klabu zao zinaposhiriki mashindano ya kimataifa, au kupitia kufanya vema wakiwa na timu za Taifa, daraja ambalo huwa na thamani zaidi.

Nipashe inaamini kuwa, kama wachezaji kutoka Afrika Magharibi au Afrika ya Kati, wamepata nafasi ya kusajiliwa na timu za Ulaya, huu ni wakati mwingine wa wachezaji wa Stars kujituma kuisaidia timu yao, lakini vile vile ni njia ya kujitengenezea ulaji binafsi.

Tunaamini kufanya vema kwa Stars katika mashindano haya, kutasaidia nchi kuwa wachezaji wengi zaidi wanaocheza soka la kulipwa na baadaye kuungana na nahodha Mbwana Samatta kuibeba Tanzania.

Na katika kuhakikisha malengo haya yanafanikiwa, wadau wanatakiwa kuwa bega kwa bega na TFF, kwa kusaidia maandalizi kwa sababu kwa kutegemea fedha kutoka kwa mdhamini mkuu wa timu hiyo pekee, hazitoshi.

Pia tunawakumbusha washangiliaji kujitokeza kwa wingi Ijumaa kuishangilia timu hiyo ili iweze kuanza vema kampeni hiyo hapa nyumbani na baadaye kuelekea Libya ikiwa na ari na morali nzuri ya kupambana.

Kila la kheri Taifa Stars, kila la kheri Watanzania kuelekea Cameroon Afcon 2021.

Habari Kubwa