Iliyoifunga Ndanda ni Yanga ya Zahera

11Nov 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Iliyoifunga Ndanda ni Yanga ya Zahera

WATANZANIA wengi wanapenda mchezo wa soka. Halafu wanapenda sana klabu za Simba na Yanga. Kupenda kwao klabu hizo, wakati mwingine kunawafanya hadi baadhi yao wanashindwa kupambanua mambo.

Kuna mwanamuziki mmoja aliwahi kuimba kuwa kupenda ni upofu. Na kweli, kwa sababu nimeona baada ya Yanga kushinda bao 1-0 Ijumaa iliyopita dhidi ya Ndanda, wanachama na mashabiki wa timu hiyo wameonekana kufurahi na kuzidi kumponda kocha wao aliyepita, Mwinyi Zahera kuwa si kocha mzuri.

Zahera huyu huyu ambaye baadhi ya wanachama walimpa uchifu, akaongoza zoezi la kuchangisha fedha, akapewa ili asajili, watu wakavaa "vipensi" kutoka majumbani kwao kwenda navyo uwanjani kwa sababu tu ya kumuunga mkono baada ya kufungiwa na Bodi ya Ligi kwa kukiuka kanuni za aina za uvaaji wa makocha.

Leo ameonekana hafai kwa sababu tu Yanga imetolewa kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho kwa kufungwa na Pyramids ya Misri.

Ukiuliza jinsi Yanga ilivyo, kama kweli wengi walitarajia kuwa ingeweza kuifunga Pyramids, mashabiki wanajibu kuwa hata kwenye Ligi Kuu timu yao imekuwa ikipata ushindi wa kusuasua.

Ukiuliza ushindi wa kusuasua upi, unajibiwa wa goli moja tu, tena yanapatikana kwa faulo, penalti au kona.

Baada ya mechi dhidi ya Ndanda FC, wanachama na mashabiki wameonekana kufurahi na kusema eti ile ndiyo Yanga waliokuwa wanaitaka.

Wanaanza kumsifia kocha, Boniface Mkwasa, kuwa ameibadilisha kidogo timu. Cha kujiuliza Mkwasa hana hata wiki kwenye kikosi, ni nini ambacho amekibadilisha?

Nilipoiangalia Yanga kwenye mechi dhidi ya Ndanda FC ni kwamba hakuna kilichobadilika.

Wachezaji ni wale wale waliokuwa wakicheza chini ya Zahera na hata aina ya matokeo ni yale yale.

Katika mechi nne za ligi ambazo Zahera ameiongoza Yanga ni kwamba imefungwa mechi moja, sare moja na kushinda mechi mbili tena kwa bao 1-0 dhidi ya Mbao FC na Coastal Union.

Kwenye mechi dhidi ya Ndanda, Yanga imeshinda tena bao 1-0, ambalo nalo pia limepatikana kwa nje ya faulo kama ilivyokuwa chini ya Zahera.

Ninachowataka wanachama na mashabiki wa Yanga ni kwamba wawe wavumilivu na wasiwe wepesi wa "kujaji" kocha aliyekuwapo na aliyeondoka kwa kipindi kifupi, tena mechi moja tu.

Wanachotakiwa ni kumpa nafasi Mkwasa na pia kocha mpya atayekuja ili atengeneze mfumo wake mpya na si kuanza kuwapa presha au kufananisha ubora wa kocha aliyepita na aliyekuwapo.

Kuanza kusifia sana au kuponda, wakati timu haijakaa sawa, itakapokuja kupata matokeo tofauti, wengine wataanza kumkumbuka kocha aliyepita na hapo tatizo litakuwa halijatatuliwa zaidi ya kuanza upya.

Bado inaonekana Mkwasa anatafuta pa kuanzia, hivyo kwenye mechi ijayo ikitokea bahati mbaya ikikosa ushindi wasiaze tena maneno, kwani inaonekana inaendelea kucheza vile vile kama ilivyokuwa chini ya Zahera na kama si goli la faulo, mechi ingeenda sare na kwa Wabongo navyowajua wangeanza minong'ono.

Yanga wamuache kwanza kocha afanye kazi yake kwenye kipindi hiki cha mpito, hadi atakapomkabidhi mwenzake kijiti.

Kutaka kuwafananisha au kuwashindanisha kwa kipindi hiki kifupi ni kutaka kuendeleza tatizo lile lile lililopo.

Habari Kubwa