Mamlaka za maji 36 zafutwa

12Nov 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Mamlaka za maji 36 zafutwa

SERIKALI imezifuta mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 36 na maeneo yake yatahudumiwa na mamlaka za makao makuu ya mikoa 25, zilizoundwa na kuongezewa majukumu ya utoaji huduma.

Hayo yalibainishwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Kilila Mkumbo, alipokuwa akitoa taarifa ya wizara juu ya maboresho hayo kwa waandishi wa habari jijini Dodoma.

Prof. Mkumbo alisema katika kiimarisha uendeshaji wa sekta ya usambazaji maji na usafi wa mazingira mijini, Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa, kwa mamalaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria, ameongeza maeneo ya huduma za maji.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5, ya mwaka 2019, ameongeza maeneo ya huduma kwa baaadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira nchini. Aidha, Waziri wa Maji ameanzisha na kufuta baadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira nchini,” alisema.

Alisema katika mabadiliko hayo kutakuwa na mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 25, katika ngazi ya makao makuu au miji mikuu ya mikoa.

Pia alisema mamlaka hizo zitahudumia halmashauri zilizopo katika miji mikuu, makao na makuu ya mikoa husika.

“Aidha baadhi ya mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira katika ngazi hii zimeongezewa maeneo ya huduma na kuunganishwa na baadhi ya miji midogo katika mikoa husika au mikoa ya jirani,” alisema.

Alizitaja baadhi ya mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira za mikoa zilizoongezewa majukumu ni Mamlaka ya Maji na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) ambayo itahudumia hadi maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga.

“Mamlaka nyingine ambayo imeongezewa majukumu ni Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Dodoma (DUWASA), ambayo nayo pia itahudumia eneo lake la jiji pamoja na miji ya Kongwa, Bahi na Chamwino,” alisema.

Nyingine ni Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) ambayo imeongezewa miji ya Kilosa na Mikumi.

“Pia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) ambayo itahudumia Halmashauri ya Jiji la Mwanza na manispaa zake na mji wa Magu, Nansio na Ngudu,” alisema.

Vilevile, alisema mamlaka za maji na usafi wa mazingira za miji midogo ya wilaya 40, zitasimamiwa na mamlaka ya maji vijijini (RUWASA) katika wilaya husika.

Alizitaja baadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira za miji midogo ya wilaya zitakazo kuwa chini ya Ruwasa ni Halmashauri ya Chemba na Kondoa.

Baadhi ya mamlaka za maji na usafi wa mazingira zilizofutwa kati ya 36, ni Kibaha WSSA, Kongwa WSSA, Chamwino WSSA, Kilosa, Kyela WSSA, Mikumi WSSA, Pangani WSSA, Magugu WSSA.

Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo, lengo ni kuongeza ufanisi na kupunguza matumizi ya fedha ili kiasi chote kiende katika utekelezaji wa miradi katika maeneo ya wananchi.

Habari Kubwa