Vyakula vyapaisha mfumuko wa bei

12Nov 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Vyakula vyapaisha mfumuko wa bei

BEI ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia Oktoba 2019 imesababisha mfumuko wa bei kuongezeka kutoka asilimia 3.4 hadi 3.6.

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Davison

Baadhi ya bidhaa hizo ni mchele, unga wa mahindi, unga wa muhogo, nyama, samaki, maziwa ya ng'ombe, mafuta ya kupikia, maharage, mihogo na viazi vitamu.

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ruth Davison, alisema jana kuwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019, umeongezeka hadi kufikia asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019.

"Hii inamaanisha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa ulioishia Oktoba 2019 imeongezeka ukilinganisha na kasi iliokuwapo kwa mwaka ulioishia Septemba 2019," alisema Davison.

Alisema kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia  Oktoba 2019 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia Oktoba 2019 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Aliainisha baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa Oktoba zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba 2018 ni pamoja na mchele kwa asilimia 6.1, unga wa mahindi kwa asilimia 20.5, unga wa muhogo kwa asilimia 10.9.

Kwa upande we nyama imeongezeka kwa asilimia 2.2, samaki kwa asilimia 16.4, maziwa ya ng'ombe kwa asilimia 3.6, mafuta ya kupitia kwa asilimia 7.0, maharage kwa asilimia 4.9, mihogo kwa asilimia 17.0 na viazi vitamu kwa asilimia 8.7.

Alifafanua zaidi kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019 umeongezeka kwa asilimia 5.1 kutoka asilimia 4.0 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019.

Kuhusu mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki, alisema Kenya kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.95 kutoka asilimia 3.83 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019.

Uganda mfumuko wa bei ulioishia Oktoba 2019 umeongezeka hadi asilimia 2.5 kutoka asilimia 1.9 kwa mwaka ulioishia Septemba 2019.

Habari Kubwa