Mdee arejea bungeni kwa kishindo, Ndugai aonya

12Nov 2019
Gwamaka Alipipi
DODOMA
Nipashe
Mdee arejea bungeni kwa kishindo, Ndugai aonya

MBUNGE wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, jana, alirejea bungeni kuendelea kushiriki vikao, huku akisababisha kishindo cha shangwe kutoka kwa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani.

Hali hiyo ilimsababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwaonya wabunge wenzake wa upinzani waliokuwa wakimshangilia mbunge huyo.

Mdee amerejea bungeni baada ya kumaliza kutumikia adhabu aliyopewa ya kutoshiriki mikutano miwili kwa kosa la kuunga mkono kauli iliyotolewa na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prod. Mussa Assad, kwamba Bunge ni dhaifu.

Aprili 2, mwaka huu Bunge liliridhia mapendekezo ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa Mdee asimamishwe kushiriki mikutano miwili ya Bunge ukiwamo Mkutano wa Bajeti wa 15 na Mkutano wa 16 uliofanyika Septemba, mwaka huu.

Jana, Mdee aliingia ndani ya mhimili huo wa kutunga sheria majira ya saa tatu asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu na kuwasalimia baadhi ya wabunge, huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge wenzake wa upinzani.

Hali hiyo, ilimlazimu Spika wa Ndugai kuwaonya wabunge waliokuwa wanashamshangilia Mdee kwa kuwaambia: “Mnaweza kumponza tena, nadhani mnanijua huwa sitanii. Nakuomba Mheshimiwa Mdee ukae tafadhari.”

Baada ya muda kidogo, Spika Ndugai alimpa nafasi Mdee kuuliza swali, ambaye alitaka kupata majibu ya serikali kuhusu fidia kwa wakati wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru), Makongo Juu na Goba wilayani Kinondoni waliopisha ujenzi wa barabara.

“Barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi-Makongo Juu-Goba iko katika mkakati wa ujenzi baada ya kero ya muda mrefu, sasa naomba kujua fidia ya Sh. bilioni tatu kwa wakazi wa maeneo hayo waliopisha ujenzi italipwa lini?” Alihoji Mdee.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema suala la fidia kwa wakazi wa maeneo hayo lipo kwa mujibu wa sheria na siyo la makubaliano.

Habari Kubwa