JPM abatilisha ufutaji shamba

12Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
JPM abatilisha ufutaji shamba

RAIS John Magufuli amebatilisha pendekezo la kufutwa shamba lenye ukubwa wa ekari 1,000 lililopo Kidunda wilayani Mvomero mkoani Morogoro linalomilikiwa na Rusimbi.

Uamuzi wa Rais Magufuli kubatilisha ufutaji shamba hilo unatokana na kubainika kuwa pendekezo lililowasilishwa la kufutwa shamba hilo kwa madai ya kutoendelezwa kutokuwa za kweli na ulilenga kumdhulumu mmiliki wake.

Akitangaza uamuzi huo wa Rais jana wilayani Mvomero, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema baada ya kufuatilia mashamba yaliyopendekezwa kufutwa, Rais Magufuli alibaini taarifa alizopelekewa za kufuta shamba Cecilia hazikuwa sahihi, hivyo kuamua kubatilisha pendekezo lililowasilishwa kwake na kumpatia haki yake mmiliki.

Kufuatia hali hiyo Waziri Lukuvi aliwaonya maofisa ardhi nchini kuhakikisha wakati wa kufanya ukaguzi/upekuzi wa mashamba yasiyoendelezwa wanazingatia haki pamoja na kufuata sheria badala ya kufanya kazi hiyo kwa upendeleo au kumwonea mtu.

Kwa upande wake Cecilia George Rusimbi alimshukuru Rais wa Magufuli kwa uamuzi wake wa kubatilisha ufutaji sahamba lake na kuuelezea uamuzi huo kuwa  umezingatia haki na kusikia kilio chake ambapo alisema umempa faraja baada ya kuhangaika sana kuhusiana na shamba hilo.

“Nimemiliki shamba tangu mwaka 1987 na kuhangaikia hati kwa muda mrefu, na nimeshangazwa kuelezwa kuwa shamba langu liko katika mpango wa kufutwa kutokana na kutoendelezwa, hii imenifanya kuishi kwa wasiwasi,” alisema Cecilia.

Habari Kubwa