Ndayiragije, Samatta waishitukia E' Guinea

14Nov 2019
Faustine Feliciane
Nipashe
Ndayiragije, Samatta waishitukia E' Guinea
  • ***Wasema dawa ni Taifa Stars kukimbiza mwanzo mwisho ili kuweza kuibuka na ushindi, lakini...

LICHA ya kukiri kutowafahamu vizuri wapinzani wao, Equatoria Guinea, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije pamoja na nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta, wamesema wanapaswa kushuka dimbani katika mechi hiyo kwa tahadhari-

Mbwana Samatta

-kubwa kutokana na wachezaji hao kulelewa katika mataifa yaliyosonga mbele kisoka barani Ulaya.

Stars itaikaribisha Equatorial Guinea kesho katika Uwanja wa Taifa kwenye mechi ya kwanza ya hatua ya makundi kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika nchini Cameroon 2021.

Wakizungumza na gazeti hili jana wakati wa Kliniki ya Soka kwa watoto iliyofanyika Shule ya Kimataifa ya Laurent jijini Dar es Salaam, Ndayiragije yeye alisema wapinzani wao hao wana wachezaji wengi waliozaliwa nje ya nchi hiyo na kupata nafasi ya kukuzwa katika vituo vikubwa vya soka barani Ulaya.

Alisema hawategemei mchezo mwepesi na watahitaji kupambana muda wote wa mchezo ili kuweza kupata matokeo chanya.

"Ninachoshukuru wachezaji wangu wapo katika hali nzuri, kila mmoja ana morali kuelekea mchezo wetu, lakini lazima tuelewe kuwa wapinzani wetu nao wana timu nzuri na wachezaji wazuri, lakini pamoja na yote ni lazima tuutumie vema uwanja wetu wa nyumbani katika kampeni hizi za kufuzu tena Afcon," alisema kocha huyo raia wa Burundi, Ndayiragije.

Aidha, alisema kikubwa ni Watanzani kuiunga mkono timu yao na kuwasapoti wachezaji wao waweze kufanya vema kwenye mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa majira ya saa moja usiku.

Kwa upande wake, Samatta alisema kwa ujumla hawawafahamu vizuri wapinzani wao kisoka, lakini hakuna mchezo mwepesi ndani ya uwanja ila hawataki kufanya makosa ya kudondosha pointi kwenye uwanja wa nyumbani kama ilivyokuwa kwenye kampeni yao ya kufuzu fainali za mwaka huu ambapo Stars ilianza kwa kutoa sare dhidi ya Lesotho katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Chamazi.

"Kwenye safari yetu, kufuzu fainali za mwaka huu tulianza na sare ya nyumbani dhidi ya Lesotho, sare ile ilitusumbua na kutupa kazi, lakini safari hii tunataka kuanza vema," alisema Samatta, ambaye pia ni nahodha katika klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji.

Samatta, alisema kwao kama wachezaji kila kitu kinaenda sawa na wanafuatilia maelekezo ya makocha wao kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo wa kesho.

Kikosi cha Taifa Stars pamoja na benchi la ufundi jana kilikuwa sehemu ya mafunzo hayo ya soka kwa watoto wenye umri kuanzia miaka 5-16 huku wakishiriki kwa pamoja uwanjani.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na kuendeshwa na Taasisi ya Afrisoccer ya jijini Dar es Salaam.