Aussems: Simba ninayoitaka ni hii

14Nov 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Aussems: Simba ninayoitaka ni hii

KOCHA Mkuu wa mabingwa watetezi, Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, amesema ameamua kuwapa wachezaji wake mazoezi tofauti kwa sababu anataka warejee Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na kasi mpya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Aussems, alisema amekuwa akibadilisha programu za mazoezi kwa nyakati tofauti kutokana na kuhitaji kuona wachezaji wote wanakuwa imara na tayari kupambana kutetea ubingwa wanaoushikilia wa ligi hiyo.

Aussems alisema pia mazoezi anayowapa yanawafanya wachezaji wote wanakuwa tayari kwa mchezo, hata kama wapo baadhi yao ambao hawajacheza mechi au wamecheza michezo isiyozidi mitatu.

"Tunajua ligi ni ngumu, kila timu inajipanga kufanya vizuri, kwa sasa kila upande hautaki kubaki nafasi za chini, ni ngumu kutumia wachezaji wale wale, na kila mechi ina mipango yake, tuko hapa kwa ajili ya kusaka matokeo mazuri na hili ndio lengo namba moja," Aussems alisema.

"Tunaongoza ligi, pia sisi ni mabingwa watetezi, ni jukumu letu kuhakikisha tunailinda heshima tuliyonayo, ni rahisi kuipoteza na ni ngumu kuifikia, lakini hakuna kisichowezekana kwenye soka."

Vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba watashuka dimbani Novemba 24, mwaka huu kucheza dhidi ya Ruvu Shooting kutoka Pwani ambayo katika mechi yake ya kwanza msimu huu iliwafunga watani wa 'Wekundu wa Msimbazi, hao, Yanga kwa bao 1-0.