Kibadeni, Mwaisabula wamchambua Chama

15Nov 2019
Focas Nicas
Nipashe
Kibadeni, Mwaisabula wamchambua Chama

KOCHA na mchezaji wa zamani wa Simba, Abdallah "King" Kibadeni pamoja na mdau na nguli wa soka nchini, Kenny Mwaisabula wametofautiana kimtazamo katika maoni yao kuhusu madai ya kuporomoka kiwango kwa kiungo wa Wekundu wa Msimbazi, Mzambia Clatous Chama.

Chama ameingia katika mjadala mzito kupitia mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu kinachotafuna kiwango chake kwa sasa ukilinganisha na ubora wa hali ya juu aliokuwa nao msimu uliopita.

Hata hivyo, wakati Kibadeni akisema kinachomtesa zaidi Chama ni kutokana na ushindani mkubwa wa namba uliopo Simba kwa sasa, Mwaisabula yeye amefunguka kuwa starehe nyingi huenda kikawa chanzo cha kiungo huyo raia wa Zambia kuporomoka kisoka.

"Pale Simba kwa sasa kuna ushindani mkubwa katika nafasi ya kiungo anayocheza Chama, kuna wachezaji kama Kahata [Francis] ambaye anakuja juu kwa sasa na pia Ajibu [Ibrahimu] na wengine, hivyo anajikuta hapati namba mara kwa mara, jambo ambalo inakuwa vigumu kuonekana kuwa katika kiwango bora," alisema Kibadeni.

Lakini Mwaisabula alisema Chama amekuwa miongoni mwa nyota wanaoelekea kuporomoka kwa kasi kiwango chake ukilinganisha na wakati anatua Simba akitokea Power Dynamos ya Zambia.

"Inaonekana starehe zinamgharimu Chama na sasa hana tena ule ubora wake dimbani. Huyu si yule Chama ninayemfahamu, si yule wa Simba wa mwaka jana, wachezaji wengi wa nje wakija Tanzania hawamalizi mwaka mmoja wanapotea dimbani, wanaendekeza starehe zaidi kuliko kazi," alisema.

Mbali na Ajibu na Kahata, lakini pia nafasi hiyo ya Chama anaweza kuicheza vizuri Mtazanzani Hassan Dilunga pamoja Sharaf Eldin Shiboub aliyesajiliwa msimu huu akitokea kwao Sudan, ambaye pia ameanza kunyoshewa kidole kuwa uwezo wake umeanza kushuka mapema.

Habari Kubwa