Chadema wamganda Jafo kujiuzulu

15Nov 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Chadema wamganda Jafo kujiuzulu

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, kujiuzulu kwa kile kinachodai kushindwa kutimiza wajibu wake katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa baraza, Patrick Ole Sosopi, alidai kitendo cha waziri huyo kutoa kauli zinazotofautiana kuhusiana na uchaguzi huo, kimeonyesha hana nia njema na uchaguzi wenyewe.

"Waziri Jafo ameonyesha sura nne tofauti, kitu kinachothibitisha ameshindwa kazi yake. Sisi kama baraza la vijana tunamtaka ajiuzulu," Sosopi alisema.

Jumapili, Jafo aliagiza wagombea wote walioenguliwa katika mchakato wa uchaguzi huo, kurejeshwa. Kauli hiyo iliibua mjadala mzito na siku iliyofuata, waziri huyo alijitokeza tena na kusema ilikuwa imetafsiriwa vibaya.

Alidai aliowalenga ni waliorejesha fomu na kuteuliwa na wasimamizi wa uchaguzi ndiyo wanaotakiwa kugombea nafasi hizo.

Vyama vingine vya upinzani vinavyomtaka Jafo kujiuzulu ni pamoja na ACT-Wazalendo na National League for Democracy (NLD), ambavyo pia vinataka mchakato wa uchaguzi huo uanze upya.

KAULI YA WAZIRI MKUU

Bungeni jijini Dodoma, jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

Waziri Mkuu alitoa rai hiyo alipojibu swali la Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula (CCM), aliyetaka kauli ya serikali baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi wakihofu kukosa haki zao za msingi za kupiga kura na kupigiwa kura.

Majaliwa alisema katika uchaguzi huo kulikuwa na maandalizi ya kujiandikisha, kuchukua na kurudisha fomu na kinachosubiriwa kuanza kwa kampeni za wagombea Novemba 17.

“Nitoe wito kwa Watanzania, kipindi kinachokuja watu waende kusikiliza sera za wagombea hao na nia thabiti ya kuwaletea maendeleo katika maeneo yao. Na kila Mtanzania apate nafasi ya kumchagua kiongozi anayemtaka,” alisema.

Habari Kubwa