Stars: Njooni Taifa, E' Guinea hawatoki

15Nov 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Stars: Njooni Taifa, E' Guinea hawatoki
  • ***Ndayiragije aanika mkakati wake akiwaita mashabiki Taifa, Boli Zozo shabiki kindakindaki awalipia wanawake...

LENGO ni ushindi nyumbani! Hiyo ndiyo kauli ya Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa Tanzania, 'Taifa Stars', Etienne Ndayiragije kuelekea mechi yao ya leo dhidi ya Equatorial Guinea kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 nchini Cameroon.

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa Tanzania, 'Taifa Stars', Etienne Ndayiragije

Taifa Stars itaikaribisha Equatorial Guinea katika mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya makundi itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam majira saa moja usiku leo.

Akizungumza na Nipashe jana, Ndayiragije alisema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika na mpaka sasa hana majeruhi yeyote katika kikosi chake huku akifurahia morali ya wachezaji kuwa juu.

"Kikosi changu kinaendelea vizuri na mazoezi, kila mchezaji morali yake ipo juu kuhakikisha ushindi unabaki nyumbani kabla ya kuelekea Libya,"alisema kocha huyo raia wa Burundi aliyerithi mikoba ya Mnigeria Emmanuel Amunike aliyetimuliwa.

Alisema tayari ameifuatilia timu hiyo na kubaini aina ya uchezaji wake huku akibainisha kuwapo kwa wachezaji wengi wazuri wanaounda kikosi hicho cha Equatorial Guinea.

"Tutaingia uwanjani tukiwa na tahadhari kubwa, lakini lengo kubwa likiwa ni kuubakisha ushindi nyumbani," alisema kocha huyo wa zamani wa Azam huku akibainisha kufurahishwa na ushirikiano mzuri uliopo kwa wachezaji wa timu hiyo ndani na nje ya uwanja.

TFF YAFUNGUKA

Kwa upande wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), limewataka wachezaji wa kikosi hicho kulipa deni kwa Watanzania kwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri nyumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamilika na waamuzi watakaochezesha mchezo huo tayari wameshawasili.

"Maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu wa kesho (leo), yamekamilika kwa asilimia 100 tunaomba wachezaji wetu wasituangushe katika mchezo huo.

"Sisi kama TFF tumejipanga kuhakikisha usalama wa kutosha unakuwapo na tunaomba Mungu atupe matokeo yenye kuridhisha," alisema Katibu huyo huku akiweka wazi wamepanga viingilio rafiki ili kila Mtanzania apate nafasi ya kuingia uwanjani kuwapa sapoti mashujaa hao wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya timu hiyo ambaye pia ni msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara, aliwataka mashabiki wa Simba kuachana na ushabiki wa timu na badala yake wawe kitu kimoja kuiunga mkono timu ya taifa.

"Mimi niwaombe mashabiki wetu wa Simba tuachane na tabia ya kwenda uwanjani kushangilia wachezaji kwa mapenzi ya timu bali tuwe kitu kimoja kushangilia timu ya nchi," alisema Manara.

Naye Boli Zozo, ambaye pia yupo ndani ya Kamati ya Uhamasishaji ya Stars, alimkabidhi Kidao fedha kwa ajili kununua tiketi 100 maalumu kwa wanawake ili wajitokeze kwa wingi uwanjani kuishandilia Taifa Stars.

"Nimejitolea kununua tiketi 100 kuwapa wanawake ili wapate nafasi ya kwenda uwanjani kushuhudia mchezo huo, yote ninaonyesha jinsi nilivyo na moyo na timu yangu ya Taifa," alisema Boli Zozo.

Habari Kubwa