Wanafunzi milioni 3 wanufaika elimu bure

16Nov 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Wanafunzi milioni 3 wanufaika elimu bure

BUNGE limeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa mpango wa elimu bila malipo, wanafunzi milioni tatu wa shule za msingi na sekondari wamesajiliwa.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, alisema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo.

Katika swali lake, Mbunge huyo alisema walimu wa shule za msingi wanafundishwa mitaala sawa na walimu awali.

"Wakati shule za awali ni za msingi sana na ndipo mtoto anapata elimu ya muhimu sana hivyo wanapswa kufundishwa namna ya kulea watoto. Je, serikali haioni umuhimu wa kuwapa kipaumbele walimu hao wa shule za awali," alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema katika kipindi cha miaka minne serikali imefanikiwa kuongeza upatikanaji wa elimu.

"Mfano kwa shule za msingi kutoka wanafunzi milioni 8.2 kwa mwaka 2015 hadi milioni 10.6 kwa mwaka 2019, hivyo ndani ya  miaka minne tumeongeza wanafunzi Milioni 2.4 kwa shule za msingi miaka hiyo,"alisema.

Kwa upande wa shule za sekondari, Ole Nasha alisema wanafunzi wameongezeka milioni 1.7 kwa mwaka 2015 hadi wanafunzi milioni 3.3 mwaka mwaka huu.

Alisema ndani ya miaka minne kuna ongezeko la wanafunzi wapya zaidi ya 600,000 na ni matunda ya elimu bila malipo.

Kadhalika, alisema serikali imeanza kuifanyia mapitio Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambapo katika mchakato huo wadau mbalimbali wakiwamo wabunge watapata fursa ya kutoa maoni yao.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alisema mfumo wa elimu umekuwa ukilalamikiwa na kukosolewa sana.

"Serikali imefanya utafiti wowote kuona kama lawama hizi zina mashiko au la,"alihoji.

Akijibu swali hilo, alifafanua kuwa serikali imekuwa ikipokea maoni mbalimbali ya wadau kuhusu mfumo wa elimu nchini na kuyafanyia kazi.

"Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu imekuwa ikifanya ufuatiliaji na kupokea mrejesho juu ya mfumo wa elimu nchini,"alisema

Alifafanua kuwa kufuatia mrejesho huo hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kwa lengo la kuboresha elimu.

"Ili kuhakikisha kuwa mfumo wa elimu unaendelea kuwa bora zaidi na wenye ushindani Kikanda na Kimataifa, Serikali imeanza kuifanyia mapitio Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambapo katika mchakato huo wadau mbalimbali wakiwamo wabunge watapata fursa ya kutoa maoni yao,"alisema.

Habari Kubwa