Kabudi: Hakuna mstaafu EAC anayedai

16Nov 2019
Gwamaka Alipipi
DODOMA
Nipashe
Kabudi: Hakuna mstaafu EAC anayedai

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema hakuna aliyekuwa mfanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliyovunjika mwaka 1977, anyeidai serikali.

Amesema waliokuwa wafanyakazi wa jumuiya hiyo wapatao 31,831 walilipwa stahiki zao zote zipatazo Sh. bilioni 117.

Aliyasema hayo jana wakati akisoma Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kueleza kuwa serikali haidaiwi hata senti moja kutoka kwa waliokuwa wafanyakazi wa jumuiya hiyo.

Prof. Kabudi alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Salome Makamba, kueleza kuwa kabla ya kuridhia itifati hiyo ni vyema serikali ikawalipa wastaafu wa jumuiya hiyo.

Makamba alisema ni vyema serikali ikalipa mafao ya wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977

"Ni jambo jema kuridhia itifaki hii inayoonesha kuwajali watumishi wa Jumuiya kwa kuwapa kinga na maslahi mazuri ya kidiplomasia. Hata hivyo, litakuwa jambo la heri zaidi kama serikali itawakumbuka wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977 (wanaotoka Tanzania) ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakidai mafao yao bila mafanikio," alisema Makamba.

Alisema wastaafu hao kupuuzwa kwa madai hayo kwa muda wote huo, kunamaanisha kuwa hawakuwa na haki au maslahi ya kidiplomasia kama watumishi wa sasa. 

"Tunaitaka serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki kupeleka hoja katika Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki ya kuzitaka nchi wanachama wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwalipa mafao wastaafu wote wa iliyokuwa jumuiya hiyo ili kuondoa dhana iliyojengeka kwamba serikali za nchi zao zimewadhulumu haki yao," alisema Makamba.

 Akijibu hoja hiyo, Prof. Kabudi alisema fedha za waliokuwa wafanyakazi wa EAC zilitunzwa nchini Uingereza na zilitumwa katika kila nchi baada ya kuvunjika.

"Hapa Tanzania tulikuwa na wafanyakazi 31,831 na waliingia makubaliano na serikali walipwe Sh. bilioni 117, na wafanyakazi hao walilipwa wote. Na walipewa miezi sita kwa yule ambaye hakuwa ameridhika apeleke malalamiko na hakuna aliyepeleka," alisema Prof. Kabudi.

Alisema baada ya kipindi cha miezi sita kupita walijitokeza wafanyakazi 5,598 wakidai Sh. trilioni 2.15, wakaenda mahakama kuu kufungua kesi lakini walishindwa.

Kabudi alisema wakaenda tena kufungua kesi katika mahakama ya rufaa lakini walishindwa, wakaenda kufungua kesi katika Mahakama ya usuluhishi ya Afrika Mashariki lakini napo walishindwa.

"Na kwa kuwa wameshindwa katika mahakama zote, serikali haiwezi kutoa hisani zaidi ya hiyo, kwa hiyo serikali haidaiwi hata senti tano, Kwa hiyo tuweke rekodi sawa kwamba hakuna mfanyakazi yoyote aliyekuwa EAC anayeidai serikali" alisema Prof. Kabudi.

Prof. Kabudi alisema orodha ya wafanyakazi wote waliolipwa ipo, baadhi yao wako hai na wengine wameshafariki dunia.

Habari Kubwa