Mkapa aeleza sababu kumteua Sumaye

16Nov 2019
Joseph Mwendapole
Nipashe
Mkapa aeleza sababu kumteua Sumaye

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa ameeleza namna alivyopata taabu kuunda baraza la mawaziri na kuwashangaza wengi alipomteua Fredrick Sumaye kuwa Waziri Mkuu wake.

Sumaye alikuwa Waziri Mkuu wa Mkapa kwa kipindi chote cha miaka 10 kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 na kuwa wa kwanza kutumikia nafasi hiyo kwa miaka yote hiyo mfululizo.

Katika kitabu chake cha 'My Life, My Purpose' (Maisha Yangu, Kusudi Langu), Mkapa anasema kuwa kabla ya kuteua baraza lake hilo, alikwenda kwa mwasisi wa taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na kumuuliza nani wanafaa na nani hawafai kuwamo kwenye baraza lake.

Anasema Mwalimu Nyerere alikataa kushiriki katika uteuzi wa baraza hilo akisema kuwa hilo ni baraza la Mkapa na hawezi kumchagulia watu wa kwenda kufanya naye kazi, hivyo alipaswa kuliunda mwenyewe.

Mkapa anasema kitu pekee ambacho Nyerere alimtaka akizingatie wakati wa uteuzi ni kuteua kwa kuzingatia usawa wa makabila na madhehebu ya dini nchini.

“Ushauri pekee alionipa Mwalimu Nyerere ni kwamba Tanzania ina makabila mengi na watu wa dini tofauti, hivyo aliniambia kuwa lazima nichague kwa kuzingatia uwiano huo,” anasema.

Mkapa anaeleza kuwa majibu hayo yalidhihirisha kwamba Mwalimu Nyerere hakupenda kuwaingilia marais, ingawa watu wengi walikuwa na mtazamo kuwa alikuwa akiwaendesha yeye na aliyemtangulia, Alhaji Hassan Mwinyi.

“Kinachofahamika ni kwamba, yeye ni Baba wa Taifa na aliiongoza nchi hii kwa miaka 20. Ingawa alikuwa akipenda sana kufuatilia masuala ya maendeleo, lakini hakutuingilia kama watu walivyokuwa wanafikiri,” anasema.

Katika kitabu chake hicho, Mkapa anasema anakumbuka sehemu pekee ambayo Mwalimu Nyerere alimshauri ni wakati alipotaka kumteua Gavana wa Benki Kuu, uteuzi ambao anakiri ulichukua muda mrefu kuamua nani wa kushika wadhifa huo.

Anasema Mwalimu Nyerere alimpigia simu na kumuuliza ni nani anayetaka kumteua kuwa Gavana wa Benki Kuu na alipomweleza kuwa ni Daudi Balali, Mwalimu Nyerere hakubisha na huo ukawa mwisho wa mazungumzo yao.

Anasema hatua yake ya kuwatupa nje ya baraza lake mawaziri wakuu wawili wastaafu, uliibua utata, hisia tofauti na iliwashangaza wengi alipoacha majina makubwa kwa wakati huo, lakini iliwafanya wengi watambue kuwa hawakuwa wanamfahamu yeye ni mtu wa aina gani.

“Nilisikia kwamba Mwalimu aliposikia mawaziri wakuu wastaafu wawili hawapo kwenye baraza langu, alisema kuwa 'sikufahamu kwamba mtu huyu ana msimamo namna hii'. Kulikuwa na sababu kwa uamuzi wangu kuhusu watu wenye sifa za kuwamo kwenye baraza langu,” Mkapa anasema.

Mkapa anaeleza kuwa lengo lake kuu lilikuwa ni kuweka matarajio ya mabadiliko kwa kuhakikisha baraza lake linatawaliwa na sura nyingi mpya huku akiwatupa nje wakongwe.

Anasema iwapo angewajumuisha Cleopa Msuya na John Malecela ambao walikuwa na nguvu kubwa kwa wakati huo, ingekuwa ngumu kwake kutetea baraza lake kuwa ni lenye kasi ya kuharakisha maendeleo kwa wakati huo.

SUMAYE WAZIRI MKUU

Mkapa anasema hatua ya kumteua Sumaye kuwa Waziri Mkuu iliwashangaza wengi kwa kuwa hawakuwa wakimtarajia kuwa na uwezo wa kushika nafasi hiyo.

Anasema faida kubwa aliyokuwa nayo na iliyomwezesha kufanya mambo yake bila kupata msukumo wowote kutoka kwa watu, ni kutokuwa na kundi wakati wa mchakato wa uchaguzi, hivyo haikuwa rahisi kupata shinikizo la kuweka watu kwenye nafasi za uteuzi.

Mkapa anasema wale waliokuwa wakijiweka karibu naye wakitaka upendeleo kutoka kwake, walikuwa wakiwekwa mbali na meneja wake wa kampeni, Ferdinand Ruhinda.

“Alikuwa akiwaambia 'kaa mbali, mwacheni Rais aongoze nchi. Tulikuwa pamoja ili tumwezeshe kushinda na afanye kazi na si kuungana naye baada ya kushinda'. Na uzuri ni kwamba, kampeni za mwaka ule hazikuwa na gharama kubwa, watu walikuwa wakichanga kwa hiyari,” anasema Mkapa.

Anasema hakulazimika kuweka watu kwenye nafasi za uteuzi kama zawadi kwa michango mikubwa waliyotoa kwenye chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, hivyo alikuwa na uhuru wa kuweka watu kwa kuzingatia umahiri wao na msaada kwa Watanzania.

Habari Kubwa